Header Ads Widget

SERIKALI YAPUNGUZA GHARAMA ZA LESENI KWA WATENGENEZA MAUDHUI MTANDAONI


Na Matukio Daima News, Dodoma


SERIKALI imetangaza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za leseni na ada za maombi kwa wabunifu, watayarishaji wa maudhui na vijana wanaotumia majukwaa ya mitandao ya kijamii nchini, katika hatua inayolenga kukuza sekta ya ubunifu na kuwapunguzia mzigo wa gharama wadau wa sekta hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Februari 12, 2026, na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu ‘MwanaFA’, wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vya utangazaji uliofanyika mjini Dodoma.

Amesema ada ya leseni kwa watayarishaji wa maudhui imepunguzwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh10,000 pekee. Aidha, kwa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepunguzwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000 na ada ya maombi kuwa Sh20,000.

“Hatua hii inalenga kuweka mazingira rafiki kwa vijana na wabunifu ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali bila kuathiriwa na gharama kubwa za awali,” amesema Mwinjuma.

Ameeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya Serikali kukusanya maoni kutoka kwa watengeneza maudhui waliolalamikia gharama kubwa za leseni zilizokuwa zikikwamisha shughuli zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Kuwe Bakari, amesema mamlaka hiyo imeanza mchakato wa maandalizi ya kuanzisha utangazaji wa redio kwa njia ya kidijitali, hatua itakayokwenda sambamba na mageuzi ya teknolojia katika sekta ya mawasiliano.








Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI