Wakala wa nishati vijijini (REA) umepiga kambi Mkoani Tanga kwa ajili ya zoezi la uhamasishaji wananchi kujiunga na huduma ya umeme.
Uhamasihaji huo umefanyika katika maeneo ya pembezoni mwa wilaya ya Tanga mjini kwenye maeneo ya sokoni ,vituo vya bodaboda pamoja na mikutano ya hadhara iliyofanyika maeneo ya ofisi za kata na mitaa lengo kubwa likiwa ni kuwapa uelewa wananchi juu ya umuhimu wa kujiunga na huduma ya umeme.
Akizungumza wakati wa uhamasishaji Afisa maendeleo ya jamii kutoka REA , ndugu Abdulrazack Mkomi alisema ,
Lengo la wakala kufika wilayani humo ni kuwafikia wananchi na kuzungumza nao juu ya umuhimu wa kutumia fursa ya upatikanaji wa huduma ya umeme ambayo ni nafuu sana na kuwahimiza kujiunga mapema na huduma hiyo ya umeme hasa wakati ambapo mkandarasi bado yupo eneo la mradi.
Aidha Mkomi amesema, utekelezaji wa miradi hii ya umeme unategemea uwezeshaji kutoka serikalini pamoja na wafadhili ambapo kwa wafadhali ili waendelea kufadhili miradi ni lazima miradi hii ya umeme iwafikie wananchi husika moja kwa moja kwa kuhakikisha wananchi wanaunganisha na kutumia umeme kwa tija ili kuboresha maisha yao na hivyo kusaidia na kuchochea uendelezaji wa miradi.
Aidha, mkomi amesema uunganishaji wa umeme kwenye miradi ya REA ni nafuu sana ambapo gharama ya uunganishaji umeme kwa ajili ya makazi ni TZS 27,000 na gharama ya uunganishaji umeme kwaajili ya mitambo au mashine pamoja na viwanda ni TZS 139,000 tu.
Halikadhalika, mkomi amewasihi wananchi kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme ambao ni nafuu kujiunganisha na kuutumia kwa tija kwa kuanzisha na kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kama shuguli za viwanda, saluni na uchomeleaji na hivyo kuwawezesha kujiajiri pamoja na kujiongezea kipato.








0 Comments