Header Ads Widget

NCHI ZINAZOONGOZA KWA RUSHWA AFRIKA, TANZANIA IKO WAPI?

 


Ufisadi unaendelea kuwa changamoto kubwa barani Afrika, huku nchi nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiorodheshwa miongoni mwa zile zilizo na alama za chini zaidi katika Kielezo cha Mitazamo ya Ufisadi cha mwaka 2025 kilichotolewa na Transparency International.

Kielezo hicho hupima nchi kwa alama kuanzia 0 (ufisadi uliokithiri) hadi 100 (uwazi na uadilifu wa hali ya juu).

Matokeo yanaonyesha kuwa Ushelisheli (Seychelles) ndiyo nchi iliyofanya vizuri zaidi katika ukanda huo kwa kupata alama 68, ikifuatiwa na Cabo Verde (62), Botswana (58) na Rwanda (58).

Msumbiji ilipata alama 21 pekee, hali inayoakisi kushuka kwa viwango kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita. Sudan, Eritrea, Somalia na Sudan Kusini zilitajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizo na alama za chini zaidi.

Kwa wastani, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara imepata alama 32, na kuifanya kuwa ukanda wenye utendaji dhaifu zaidi duniani katika suala la kudhibiti ufisadi.

Tangu mwaka 2012, ni nchi saba tu katika ukanda huo zimeonyesha maendeleo ya kuboresha alama zao kwa kudhibiti viwango vya ufisadi.


AFIRIKA MASHARIKI IKO WAPI?


Afrika Mashariki inaelekea kuwa eneo linalolemewa katika udhibiti wa ufisadi na rushwa, huku Rwanda ikiendelea kuongoza kukabiliana na ufisadi wakati nchi jirani zinapambana kudhibiti kudorora kwa uwazi.

Sudan Kusini na Somalia kwa mara nyingine tena zimeorodheshwa kuwa nchi fisadi zaidi duniani na hata Afrika Mashariki zikipata alama 9 tu kati ya 100 katika Fahirisi ya Mitazamo ya Ufisadi ya 2025 iliyotolewa Jumanne na Transparency International.

Mataifa hayo mawili yaliyoathiriwa na mizozo yapo mkiani kabisa mwa fahirisi, yakiwa na alama sawia za chini kabisa na kufuatiwa kwa karibu na Venezuela, iliyopata alama 10.


Kulingana na Transparency International, nchi ambazo mara kwa mara zimekithiri ufisadi huwa na sifa zinazofanana: kukosekana kwa utulivu kwa muda mrefu, taasisi za serikali zilizodhoofika, maeneo yenye vikwazo vya kiraia, na mifumo ya ufadhili iliyoimarishwa ambayo inaruhusu rushwa kustawi na matokeo kidogo.

Katika mazingira kama haya, mashirika ya uangalizi yanatatizika kufanya kazi, sheria za kupambana na ufisadi hazitekelezwi vizuri, na rasilimali za umma mara nyingi huelekezwa kwa manufaa ya kibinafsi.

"Rushwa haiwezi kuepukika, lakini kukosekana kwa uongozi shupavu kunaifanya kuhisi hivyo," alisema François Valérian, Mwenyekiti wa Transparency International, katika taarifa iliyoambatana na ripoti hiyo.

Burundi ina alama 17, ikifuatwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na alama 20, na ikiwa kipimo ni asilimia 100.

Kima cha Kimataifa kimeiweka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nafasi ya 163, na Burundi nafasi ya 167.

Uganda nayo imetajwa kuwa na vitendo vya ufisadi vingi ikiwa na alama 25, huku kimataifa ikiwa katika nafasi ya 148.

Katika Jumuiya ni ya tano ikibainika ina vitendo vya rushwa zaidi ukilinganisha na Kenya na Tanzania.

Taifa la Kenya limeorodheshwa ya sita kuwa na viwango vya juu vya ufisadi mwingi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo, haijaonyesha dalili za mafanikio ya maana katika kuukabili, kwa mujibu wa Ripoti ya Kielezo cha Mitazamo ya Ufisadi ya mwaka 2025 iliyotolewa na Transparency International.

Ripoti hiyo, iliyochapishwa Februari 10, inaonyesha kuwa alama ya Kenya imeshuka hadi pointi 30 kati ya 100, kutoka 32 mwaka 2024.

Katika orodha ya mataifa 181 yaliyopimwa, Kenya imeshika nafasi ya 130 ikiwekwa katika kundi la nchi ambako ufisadi unaendelea kuwa tishio kubwa, huku juhudi za kuudhibiti zikionekana kuwa na mafanikio haba.

Kwa mujibu wa tathmini ya Transparency International, Kenya iko nyuma ya baadhi ya majirani zake wa Afrika Mashariki.

Aidha, alama ya Kenya iko chini ya wastani wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambao ni pointi 32 hali inayoifanya iwe miongoni mwa nchi zenye utendaji dhaifu katika eneo ambalo tayari linapambana na changamoto kubwa ya ufisadi.

Rwanda, inayotajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya chini vya ufisadi katika Afrika Mashariki, imeonyesha dalili za kuimarika tangu mwaka 2024.

Madeleine Nirere, ambaye haegemei upande wowote, alisema utashi endelevu wa kisiasa unasalia kuwa nguzo muhimu katika juhudi za kupambana na ufisadi nchini Rwanda.

"Kuna dhamira kubwa ya kisiasa, na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma. Hili lina jukumu kubwa," alisema. "Rwanda imepitisha mtazamo kamili wa kupambana na rushwa, ikiungwa mkono na ushirikishwaji wa raia, sheria madhubuti za kupambana na rushwa, na uwekaji huduma kidijitali."


NAFASI YA TANZANIA 



Tanzania, kwa upande wake, imerudi nyuma kidogo ikilinganishwa na hatua ilizopiga mwaka uliotangulia.

Imeshuka kutoka alama 41 mwaka 2024, ikitafsiriwa kuwa mwaka 2025 visa vya ufisadi vilikithiri zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2025, imeshika nafasi ya pili Afrika mashariki kwa taifa ambalo lina viwango vya chini vya ufisadi kwa alama ya asilimia 40, na orodha ya mataifa 181 yaliyopimwa ilishika nafasi ya 84.

Ingawa kunaonyesha kudorora kwa uwazi Tanzania bado iko mbele ya Kenya na Uganda katika mienendo ya kukomesha rushwa.

Ikilinganishwa na Rwanda, Tanzania imeshindwa kukabiliana na ufisadi na vitendo vya rushwa kikamilifu.

Alama 40 ya Tanzania ipo juu ya wastani kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, ambao ni 32/100.

Nafasi ya Tanzania katika udhibiti wa ufisadi imekuwa wastani wa 96.25 kuanzia 1998 hadi 2025, ikipata kiwango cha juu kabisa cha 126.00 mwaka 2009 na kiwango cha chini kabisa cha 71.00 mwaka 2002.

NCHI ZILIZOLEMEWA NA UFISADI

Hali mbaya zaidi ilibainika nchini Burundi, pamoja na Somalia na Sudan Kusini, ambazo zimetajwa kuwa katika hali ya hatari kubwa ya ufisadi kukolea.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Transparency International Rwanda Apollinaire Mupiganyi alibainisha kuwa CPI ya 2025 imegundua kichocheo kikubwa kilichoongeza ufisadi ni kudhofika kwa uwajibishaji, kuingiliwa kwa kisiasa na kuongezeka kwa uvumilivu kwa tabia zisizo za kimaadili katika nchi kama hizo.

Nchi zote hizo zimetajwa hapo juu kuwa zimelemewa na ufisadi zipo katika kundi la Afrika Mashariki ambalo limemulikwa kwa uongozi kutowajibika kuhakikisha mali ya umma haikamuliwi.

UFISADI UNAPOONEKANA MACHONI.


Athena Charanne Presto, mwanasosholojia kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, anasema kuwa mitandao ya kijamii imegeuza taarifa za kisiasa kuwa ushahidi unaoonekana.

"Wakati ufisadi unapotajwa kwenye ripoti au kesi za kisheria, huwa ni jambo la mbali. Lakini watu wakiona kupitia simu zao kwenye picha za majumba ya kifahari, magari ya kifahari, na maisha ya anasa ufisadi unakuwa halisi."

Ubadhirifu wa pesa za umma miongoni mwa viongozi hasa barani Afrika Gen- Z wanaichukulia kama dhihaka kwa maisha magumu ya watu wa kawaida.

Na likiwakoroga vijana wa kizazi kipya ambao katu hawataki kuona wala kuskia dhulma matokeo yake ni maandamano ambayo yanakwamisha shughuli za kawaida na hata wengine wako radhi kupoteza maisha yao wakipigania uwazi na uhuru.

Mambo kama hayo pia yalijitokeza Ufilipino, ambapo vijana walihusisha maisha ya kifahari ya wanasiasa na ufisadi kwenye miradi ya kuzuia mafuriko, ambayo watu wengi hufa kutokana nayo.

Ripoti hiyo pia inaashiria kuongezeka kwa mwamko wa kiraia dhidi ya ufisadi hasa nchini Kenya na hivi majuzi Tanzania.

Maandamano ya kupinga serikali katika maeneo mbalimbali duniani yanaonyesha kuwa wananchi wamechoshwa na uongozi usio na uwajibikaji, na sasa wanadai mageuzi ya kweli.

PENDEKEZO NI LIPI?

Ripoti ya CPI inaonyesha kuwa wastani wa alama duniani umeshuka hadi 42 kati ya 100, kiwango chake cha chini zaidi katika zaidi ya muongo mmoja.

Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa Transparency International, François Valérian, alionya kuhusu kile alichokiita kupuuzwa kwa viwango na misingi ya kimataifa na baadhi ya mataifa.

"Katika wakati huu tunaposhuhudia baadhi ya nchi zikidharau kanuni za kimataifa, tunatoa wito kwa serikali na viongozi kuongoza kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha mustakabali bora kwa watu duniani kote," alisema.

Shirika hilo la kimataifa linahimiza kufufuliwa kwa dhamira ya kisiasa katika vita dhidi ya ufisadi, kulindwa kwa nafasi ya kiraia ili wananchi waweze kushiriki bila hofu, na kuzibwa kwa mianya ya usiri inayowezesha vitendo vya kifisadi kufichwa.

Kwa ujumla, matokeo haya yanatoa taswira ya changamoto inayoendelea na yanatoa mwito kwa hatua madhubuti, si maneno matupu, katika mapambano dhidi ya ufisadi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI