Na Josea Sinkala, Mbeya.
Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) ya Mbeya (Mbeya DC), imepitisha rasimu ya mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa kupanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 72.4 kutoka katika vyanzo mbalimbali.
Miongoni mwa vyanzo hivyo ni pamoja na mapato ya ndani na ruzuku ya Serikali kuu kwa ajili ya kugharamia mishahara (50.6b/=), matumizi ya kawaida yaani 'OC' (5.2b/=), maendeleo (13.8b/=), vyanzo fungiwa kama vile 'CHF', 'User Fee', NHIF, na Michango ya jamii (2.6b/=).
Akisoma mapendekezo ya rasimu ya bajeti mbele ya DCC, Mkuu wa divisheni ya Mipango na Uratibu Francisca Nzota, amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri inakadiria kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 8.4, ambapo shilingi bilioni 5.8 zinatokana na mapato halisi (own source proper) na shilingi bilioni 2.6 kutoka vyanzo fungiwa.
Amesema ili kufanikisha malengo ya mpango wa maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027, amesema Halmashauri ya Mbeya imekadiria kutumia jumla ya shilingi bilioni 13.8 kwa ajili ya kutekeleza programu na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa mujibu wa bi. Francisca, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 2.3 ni mapato ya ndani na shilingi bilioni 11.5 ni ruzuku kutoka Serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Mpango wa maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, unalenga kuendeleza juhudi za Serikali katika kuimarisha Halmashauri hiyo kwa kujiongezea uwezo wa kutenda kazi, kutathmini na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo, kuwezesha wananchi kutambua fursa na vikwazo vilivyopo katika maeneo yao ili kupanga na kutekeleza mipango yao, kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kama ilivyoelezwa katika Dira ya maendeleo ya Taifa awamu ya pili, kutekeleza miradi ya maendeleo inayoendelea na kukusanya mapato pamoja kubuni vyanzo vipya vya mapato ya Mbeya DC.






0 Comments