Nyamagana — Maofisa wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanatarajiwa kupatiwa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo katika kulinda na kuendeleza hifadhi za misitu ya mikoko, hatua inayolenga kuimarisha ulinzi wa rasilimali hizo nyeti na kukabiliana na uharibifu unaotokana na shughuli haramu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza, Februari 05, 2026, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, Amina Makilagi, amesema mafunzo hayo yataongeza tija, maarifa na weledi wa maofisa wa uhifadhi, akisisitiza kuwa misitu ya mikoko ni mhimili muhimu katika ulinzi wa fukwe za bahari, ikolojia ya majini na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya pwani.
Akihitimisha hotuba yake, Mgeni Rasmi ametoa pongezi za kipekee kwa Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, kwa namna anavyothamini ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini. Amesema juhudi hizo zinaonekana wazi kupitia usimamizi thabiti wa hifadhi, pamoja na kasi ya utekelezaji wa programu za upandaji miti katika kanda na wilaya zote nchini.
Aidha, Mgeni Rasmi amesifu kwa kiwango kikubwa ushirikiano uliopo kati ya askari na maofisa wa TFS ngazi ya kanda na wilaya na ofisi yake, akieleza kuwa mshikamano huo umeimarisha utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi na kudhibiti uharibifu wa misitu, hususan katika maeneo nyeti ya mikoko.
Kwa upande wake, Kamanda wa TFS Kanda ya Ziwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ebrantino Mgiye, amemshukuru Kamishna wa Uhifadhi kwa kuridhia kibali cha mafunzo hayo, akibainisha kuwa ulinzi wa misitu ya mikoko una mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda fukwe za bahari na kudumisha bioanuwai.
Naye Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji (MPC), SACP Ndagile Azaria Makubi, amesema chuo hicho kimejipanga kutoa mafunzo yenye viwango vya kitaalamu, yatakayowawezesha washiriki kupata mbinu na stadi za kisasa za kukabiliana na uhalifu wa majini na kusimamia kikamilifu hifadhi za mikoko.










0 Comments