Na. Jacob Kasiri - TANAPA.
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kuwahifadhi na kuwalinda kwa jitihada kubwa Faru weusi (Black rhino) waliokuwa hatarini kutoweka mwishoni mwa miaka ya 1990 kutokana na ujangili uliokithiri pamoja na kushamiri kwa biashara haramu ya pembe zake katika bara la Asia.
Kati ya Hifadhi za Taifa 21 zinazosimamiwa na (TANAPA), wanyamapori hao (Faru Weusi), wakiwa ni miongoni mwa wanyama waliomo katika kundi linalojulikana kama “The Big Five” wanapatikana katika Hifadhi za Taifa Mkomazi na Serengeti.
Kwa leo tujikite kuangalia tabia chache za kipekee zitakazokuachia kumbukumbu na tabasamu lisilosahaulika maishani mwako utakapofanya utalii wa Faru katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi.
TABIA HIZO NI PAMOJA NA;
• Faru Weusi wanaweza kushambulia kitu chochote kilichopo mbele yao hata bila sababu za msingi, kwao wakidhani ni adui, hivyo kuamua kujibu mapigo ili wajilinde na kukabiliana na adui kwa wakati huo.
• Faru weusi pia, wana sifa ya kuwa wakali na wenye hasira za haraka mithili ya binadamu mwenye msongo wa mawazo, wakati mwingine hasira hizo hufananishwa na nyoka aliyeshtushwa na kuamua kugonga chochote kilichopo mbele yake, nyuki au dondora wapokuwa katika masega yao. Japo hakuna kiumbe hai kilichothibitika kisayansi kuwa ndicho chenye hasira za haraka zaidi duniani.
• Wanaweza kukimbia kwa kasi hadi kilometa 55 kwa saa wakigutushwa na sauti ya kitu chochote au mvumo wa upepo wakidhani kuna hatari hata kama kitu hicho sio tishio kwao.
• Wakati mwingine hushambulia hadi vivuli vyao wakidhani ni adui anataka kuwadhuru.
SABABU ZA TABIA HIZO NI:
Wanyamapori hao wana uoni hafifu nyakati zote iwe mchana au usiku hivyo, kutegemea zaidi kunusa na kusikia, kwa muktadha huo muda wote huchukua tahadhari.
Kwa dondoo hizi na nyingine kedekede za Faru weusi - Mkomazi ndio jibu lako.






0 Comments