Na Matukio Daima Media ,Iringa
MJUMBE wa kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (MCC) Hamad Chande anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 49 ya kuzaliwa yatakayofanyika Idodi wilaya ya Jimbo la Isimani.
Huku wananchi na wana CCM wote wa wilaya hiyo na mkoa wa Iringa wakiombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo yatakayofanyika February 5 mwaka huu huku yakilenga kuenzi historia, mafanikio na utekelezaji wa ahadi za maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Anord Mvamba, amesema sherehe hizo ni fursa muhimu kwa chama kukutana na wananchi ili kutathmini safari ya miaka 49 ya CCM, kusherehekea mafanikio yaliyopatikana pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa chini ya uongozi wa chama hicho.
“Chama Cha Mapinduzi kinapenda kuwakaribisha wananchi wote na wana-CCM kushiriki Maadhimisho ya Miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM Maadhimisho haya yatafanyika Tarafa ya Idodi, Kata ya Idodi, Jimbo la Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini. Tunakwenda kusherehekea mafanikio ya miaka 49 tangu kuanzishwa kwa chama chetu,” amesema Mvamba.
Aidha, Mvamba ameeleza kuwa CCM inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa barabara ya Iringa – Msembe ambao unaendelea kutekelezwa kama ilivyoahidiwa. Lami inajengwa na hatua kubwa tayari imefikiwa. Pia Tarafa ya Idodi imechaguliwa kwa kuwa kila kata ina Kituo cha Afya, na kituo bora zaidi katika mkoa wa Iringa kinapatikana Idodi,” ameongeza.
Mvamba pia ametoa shukrani kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa chini ya Mwenyekiti wake, Daudi Yasin, kwa kuichagua Wilaya ya Iringa Vijijini kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, akisisitiza kuwa chama kimejipanga kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika kwa amani na furaha.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa kwa uamuzi huo. Sisi kama chama tumejipanga vizuri kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika kwa utulivu, amani na mshikamano,” amesema.
Ameongeza kuwa asilimia kubwa ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika Mkoa wa Iringa inapatikana Kata ya Idodi, hali inayowapa wananchi fursa ya kujionea maendeleo yanayofanywa na serikali kupitia maadhimisho hayo.







0 Comments