Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Imeelezwa kuwa ukusanyaji wa chuma chakavu na taka za plastiki una nafasi kubwa ya kutengeneza ajira kwa vijana kutokana na takataka hizo kuwa na soko kubwa kwenye viwanda mbalimbali nchini.
Afisa Miradi Mwandamizi wa Shirika la Catholic Relief Services (CRS), Simon Mwanjela alisema hayo wakati waandishi wa habari wakitembelea maeneo mbalimbali ya vijana hao wajasiliamali wanaojihusisha na uchumi rejeshi kwa kukusanya taka za chima na plastiki na kuziuza viwandani ili zitengenezwe bidhaa nyingine.
Mwanjela alisema kuwa shirika hilo linatekeleza mradi huo ambao unalenga kuongeza ubora wa maji ya ziwa Tanganyika ili kuzuia taka hizo zisiingie ziwani bali zikusanywe na kurudishwa tena kwenye matumizi na kwamba kupitia mradi wa VOICES kwa ufadhili wa Jumuia ya Ulaya wanatarajia kuwapatia ruzuku vijana wanaojishughulisha na mpango huo ili kupanua shughuli zao.
Mmoja wa vijana wanaohusika na ukusanyaji wa taka za plastiki katika tarafa ya Nguruka wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Nassir Majengo alisema kuwa ukusanyaji wa bidhaa za chupa zilizotumika umetengeneza ajira kubwa kwake na vijana wenzake kwani katika kijiwe chake alichofungua ameajiri vijana 15 ambao wanatumika kukusanya mabaki ya chupa za plastiki zilizotumika kutoka vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo.
Kwa upande wake Idrisa Mussa anayekusanya chuma chakavu katika eneo la Mwandiga Halmashauri ya wilaya Kigoma alisema kuwa alianza kukusanya chuma chakavu miaka 10 iliyopita lakini kwa sasa imekuwa ajira kubwa ambapo amefungua vituo saba vya kukusanya chuma chakavu na anao vijana 30 ambao kila siku wakiamka kazi yao ni hiyo.
Hata hivyo anasema kuwa kazi hiyo ili kufikia hatua ya kuuza chuma hicho kiwandani inahitajika mtaji ambapo kuweka kujaza semitrela moja kila mwezi inahitajika wastani wa milioni 10 lakini akiuza anapata hadi milioni 30 ambapo akilipa mishahara ya watu wake anabaki na hela ya kutosha hivyo kupata mtaji kuifanya biashara kwa ukubwa wake ndiyo changamoto kubwa.
Mwisho.





0 Comments