Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo amehamasisha waajiri nchini kutoa kipaumbele kwa vijana wanaojitolea katika maeneo ya kazi ili kuimarisha mahusiano mazuri pamoja na morali ya kazi kwa vijana hao.
Amesema hayo leo Januari 9, 2026 katika ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo na uboreshwaji mwongozo wa watarajali wa Mwaka 2017 uliowakutinisha Waajiri wote nchini Jijini Dar es salaam.
Aidha, Naibu Waziri kisuo amewataka waajiri kuondoa urasimu katika kuwapokea vijana kwa ajili ya mafunzo ya kazi. Pia amesema kuwa vijana wanahitaji sana fursa hizo ili waweze kupata ujuzi wa vitendo, kujiamini na kujiandaa na ushindani uliopo katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Mafunzo ya Uzoefu katika kazi ni nyenzo muhmu katika kujenga taifa lenye nguvu ya uchumi na kijamii.
Imani yangu mshikamano huu mliokuwa nao tutafanikisha kuandaa vijana wenye ujuzi, nidhamu na maadili ya kazi kwa manufaa ya taifa letu,” amesema
Vilevile, ametoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwa waajiri na wasisite kuomba nafasi zinazotangazwa na wajitokeze ili kuonesha uwezo wao. Ameongeza kuwa, Mafunzo hayo ni daraja la mafanikio yao ya baadae
Akizungumza Awali, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus amewashukuru wadau wote kwa kuitikia wito wa serikali na kushiriki kikamilifu katika kikao kazi hicho kwa kuwa watakuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira nchini.
Kikao kazi hicho kimelenga kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa waajiri waliofanya vizuri katika utekelezaji wa programu ya mafunzo Tarajali (Internship); kupata jukwaa la pamoja ili kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuimarisha utekelezaji wa Programu hiyo ili iwe na tija na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.











0 Comments