NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, jimbo na kata kuzingatia Katiba, sheria na maelekezo ya Tume ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, amani na ufanisi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi yanayofanyika Mkoani Iringa kuanzia tarehe 24 hadi 26 Januari, 2026, Mhe. Mwambegele alisema kuwa uchaguzi ni mchakato unaohitaji umakini mkubwa katika kila hatua ili kuepusha malalamiko na migogoro isiyo ya lazima.
Alisema kuwa uteuzi wa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa jimbo na kata, pamoja na maafisa uchaguzi, umezingatia weledi, uzoefu na uaminifu kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024.
“Ninawasisitiza kuheshimu viapo mlivyoapa na kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni zake pamoja na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi,” alisema Mhe. Mwambegele.
Aidha, alisema kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, jukumu la kusimamia na kuratibu uchaguzi ni la Tume, lakini utekelezaji wake unahitaji uwepo wa waratibu na wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi mbalimbali.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yamelenga kuwajengea uwezo washiriki katika usimamizi, uratibu na uendeshaji wa uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Peramiho na Udiwani katika Kata ya Shiwinga, huku mada kumi zikiwasilishwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto za kiuchaguzi.
Aliwataka washiriki kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili pamoja na wadau wengine, sambamba na kufanya utambuzi wa mapema wa vituo vya kupigia kura ili kubaini mahitaji maalum na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani.
Pia aliwakumbusha umuhimu wa kuajiri watendaji wa vituo wenye sifa, kuhakiki vifaa vya uchaguzi, kuvipatia vyama vya siasa orodha ya vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kupanga mawakala, pamoja na kuhakikisha vituo vinafunguliwa saa 1:00 asubuhi siku ya uchaguzi.
Kwa upande wake, aliwahimiza washiriki wapya kujifunza kwa haraka na kutumia uzoefu wa wenzao, huku waliobobea wakitumia fursa hiyo kubadilishana maarifa mapya.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa magunzo hayo Dany Tweve alisema mafunzo hayo kwao ni chachu ya kuwakumbusha kwenda kuongeza umakini katika utendaji kazi wao pia kwenda kuwajibika kuwakumbusha wananchi wajibu wao kushiriki uchaguzi huo pia kujitokeza kusikiliza wagombea wote wakati wa kampeni.








0 Comments