Header Ads Widget

TMDA WATOA UFAFANUZI KUHUSU MATUMIZI YA DAWA ZENYE KIAMBATA HAI CHA LEVONORGESTREL


Na. Matukio Daima Media App.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya dawa zenye kiambata hai (active ingredient) kijulikanacho kitaalam kama levonorgestrel.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa Umma iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo imebainisha kuwa, 

Ufafanuzi huo unatolewa kufuatia taarifa iliyorushwa hewani na vyombo vya habari vikinukuu matumizi holela ya dawa husika ambayo ilionesha kuchanganya maelezo ya dawa za aina mbili tofauti ambazo zilikuwa zikizungumziwa kwa wakati mmoja.

Katika taarifa hiyo iliyojichanganya ilionekana kuainisha kwamba dawa tajwa ikiwa ni pamoja na dawa maarufu iliyopo kwenye soko ijulikanayo kama P2 hutumika kwa ajili ya kutoa mimba.

"Taarifa sahihi ni kwamba dawa zenye kiambata cha levonorgestrel zinatumika kuzuia mimba baada ya kufanya tendo la ndoa na kuwa na wasiwasi wa kupata ujauzito kwa dharura (emergency contraceptive). 

Dawa hii imethibitishwa na TMDA kutumika kama mojawapo ya njia za uzazi wa mpango na hutakiwa kutumika ndani ya masaa 72 baada ya tendo la ndoa (unprotected sex).

Pamoja na ufafanuzi wa matumizi ya levonorgestrel, madhara ya dawa hii ni pamoja na kuharibu mzunguko wa hedhi, kupata hedhi nyepesi au nzito, kuwahi au kuchelewa kupata hedhi, maumivu ya tumbo, kuharisha, kizunguzungu, kuchoka, kupata gesi tumboni na kuumwa kichwa.

Dawa hii pia haizuii magonjwa ya zinaa (sexually transmitted infections – STIs).

Aidha, dawa ambayo imekuwa ikitumika kinyume na taratibu za kitabibu ni misoprostol ambapo watumiaji huitumia kwa ajili ya kutoa mimba. 

Hata hivyo, matumizi ya misoprostol kwa ajili ya kutoa mimba bila ushauri wa wataalam wa afya (misuse) ni ya hatari na TMDA inayakemea na kuendelea kuelimisha umma kutoitumia kwa makusudi haya kutokana na madhara yake kiafya.

Matumizi yaliyoidhinishwa ya misoprostol ni pamoja na kuzuia vidonda vya tumbo (stomach ulcers prevention), kutoa mimba (medical abortion), kusaidia wakati wa kujifungua (labor induction and cervical ripening), kuzuia kutoka kwa damu baada ya kujifungua (postpartum haemorrahge) na kusaidia baada ya mimba kutoka kwa bahati mbaya (miscarriage management). 

Madhara ya kiafya ya misoprostol ni pamoja na; kuharisha, maumivu ya tumbo, kichefuchefu, kutapika, kujaa gesi tumboni, kichwa kuuma, kutetemeka, kutokwa damu ukeni, moyo kwenda mbio, kushindwa kupumua, kutoka vipele, kuharibu mzunguko wa hedhi, kupata homa na kizunguzungu. 

Hata hivyo, dawa hii haitakiwi  kutumika endapo mama ni mjamzito. 

TMDA inaendelea kuwataka wananchi wafuate maelekezo ya wataalam wa afya kabla na baada ya kutumia dawa zote ili kulinda afya zetu wote." Imebainisha taarifa hiyo  kwa Umma.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI