Header Ads Widget

KAPALATA AIOMBA SERIKALI KUCHUKUA HATUA ZA MAPEMA KUIOKOA MIIJI INAYOZUNGUKA MIGODI*


Aekeza kuwa miji mingi duniani kudorora na kufa kiuchumi baada ya migodi kufungwa*

Ataka viwanda, ajira na miundombinu ianzishwe sambamba na uwekezaji wa madini*

Waziri Mavunde apongeza ushauri wa kitaalamu na mtazamo wa muda mrefu*

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Neto Paul Kapalata, ameitaka Serikali kuweka Sera na miongozo madhubuti itakayohakikisha utoaji wa leseni kubwa za uchimbaji madini unaambatana moja kwa moja na wajibu wa kuendeleza miji inayozunguka migodi, ili miji hiyo iendelee kuwa na uhai wa kiuchumi na kijamii hata baada ya rasilimali za madini kuisha.

Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati hiyo, Mheshimiwa Kapalata amesema uzoefu wa kimataifa unaonesha kuwa utegemezi wa miji mingi kwenye uchumi wa madini pekee umesababisha kudorora kwa shughuli za kijamii na kiuchumi mara tu miradi ya uchimbaji inapofikia tamati, jambo linaloacha athari kubwa kwa wananchi na Serikali.

“Miji mingi duniani imekosa uendelevu baada ya migodi kufungwa kwa sababu ya kukosekana kwa mipango mbadala ya maendeleo. Mfano chanya ni Johannesburg (Egoli) nchini Afrika Kusini, ambayo iliweza kukua na kuendelea baada ya shughuli za madini kutokana na sera thabiti za kuendeleza sekta nyingine za uchumi,” amesema Mhe. Kapalata.


Ameeleza kuwa changamoto hiyo inatokana na kukosekana kwa mikakati ya muda mrefu inayolenga kuanzisha shughuli mbadala za kiuchumi, ikiwemo viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, biashara, huduma na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya kijamii na kiuchumi itakayodumu hata baada ya rasilimali kuisha.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kapalata amefafanua kuwa utafiti wa madini ni shughuli inayohitaji uwekezaji mkubwa kutokana na matumizi ya sayansi, teknolojia ya kisasa na rasilimali watu wenye utaalamu wa hali ya juu. Hata hivyo, amesifu hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Madini kwa kuonesha ujasiri na dhamira ya kuwekeza katika tafiti za kina za madini kwa maslahi ya muda mrefu ya Taifa.

Ametoa mapendekezo ya kitaalamu ya kuimarisha tafiti za madini kwa kuzingatia upangaji makini, matumizi ya takwimu sahihi za kijiolojia na uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama. Aidha, ameitaka Wizara ya Madini kuanzisha kitengo maalum cha Minerals Development kitakachosimamia tafiti, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, pamoja na kuyaandaa maeneo yenye rasilimali kwa ajili ya uwekezaji kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, amempongeza Mheshimiwa Kapalata kwa mchango wake wa kitaalamu na ushauri unaolenga kuijenga sekta ya madini kwa mtazamo wa maendeleo endelevu ya Taifa.


“Ninampongeza Mheshimiwa Kapalata kwa ushauri wake wa kitaalamu unaoangalia maslahi ya muda mrefu ya sekta ya madini na maendeleo ya miji inayozunguka migodi. Huu ni mchango muhimu katika kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi hata baada ya uchimbaji kukamilika,” amesema Waziri Mavunde.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Subira Mgalu, amesema Kamati itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini kuhakikisha sekta ya madini inakuwa kichocheo cha maendeleo endelevu ya Taifa na ustawi wa wananchi, si tu wakati wa uchimbaji bali pia baada ya rasilimali za madini kumalizika.

Amesisitiza kuwa usimamizi na ushauri wa kitaalamu wa Kamati utaendelea kuimarika ili kulinda maslahi ya Taifa katika sekta ya madini, ambayo ni nguzo muhimu ya uchumi wa nchi.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI