Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Wakati zoezi la usajili wa kaya masikini katika mpango wa bima ya afya kwa wote umeanza wiki hii nchini Kote MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amewaonya viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa kutoingiza majina ya walengwa wasio na sifa katika zoezi hilo.
Balozi Sirro alisema hayo akizungumza kwenye mkutano wa baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya Kasulu mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa katika awamu ya kwanza ya usajili kwa ajili ya Bima ya afya kwa wote unalenga kaya masikini hivyo ni lazima walengwa ambao takwimu zao zipo kwenye mamlaka za serikali za mitaa zitumike badala ya kuingiza majina mpya na yasiyo na sifa.
Mkoa wa Kigoma unaelezwa kuwa na walengwa 120,000 kutoka kaya masikini zinazonufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) na kwamba kwa awamu ya kwanza kaya 66,800 zinatarajia kusajiliwa kunufaika na mpango wa bima ya afya kwa wote ambapo Mkuu wa mkoa amehimiza viongozi kuhamasisha walengwa kujitokeza ili kuandikishwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Kasulu, Isack Mwakisu amewataka madiwani, watendaji na wenyeviti wa serikali za vijiji kutoingiza masuala ya kisiasa kwa kuanza kushinikiza kusajiliwa kwa watu wasio walengwa wa kundi la kaya masikini kwani taarifa na takwimu za watu hao zipo hadi kwenye ngazi za serikali za vijiji hivyo takwimu na taarifa hizo ndizo zinazopaswa kutumika.
Akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya Kasulu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Samuel Kadogo alisema kuwa wamepokea maelekezo hayo na watasimamia kwa karibu kuona walengwa wa kaya masikini wananufaika na hakutakuwa na uchakachuaji wa kuingiza majina mapya Zaidi yay ale yaliyopo kwenye kanzi data zilizopo.










0 Comments