Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua rasmi mfumo wa kidijitali wa kuhudumia wateja unaotumia Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), maarufu kama Bwana Bumu na Bibi Bumu, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa bodi hiyo, Bahati Singa, alisema mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya mikopo na unatumia teknolojia ya kisasa ya akili hunde kuchakata taarifa kwa haraka na kwa usahihi.
Alieleza kuwa hapo awali bodi ilikuwa ikitumia njia mbalimbali kuwafikia walengwa wa mikopo, hali iliyosababisha kuwafikia wanufaika wachache waliokuwa kati ya 5,000 hadi 6,000 pekee.
Hata hivyo, kutokana na maboresho ya mifumo, kwa sasa bodi inaweza kuwafikia zaidi ya walengwa 10,000 na kwa kutumia mfumo huo mpya, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia kati ya walengwa 100,000 hadi 200,000.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Bili Kiwia, alisema uzinduzi wa Bwana Bumu na Bibi Bumu ni hatua kubwa katika mageuzi ya utoaji wa huduma kwa wateja, kwani mfumo huo utakuwa unatoa huduma masaa 24 kwa siku saba kwa wiki, mwaka mzima, hali itakayosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa wanufaika.
“Hatupendi kuwa watumiaji wa teknolojia zinazobuniwa nje ya nchi pekee, bali tunajivunia kuanzisha mfumo huu ndani ya nchi kwa kutumia wataalamu wetu,” alisema Kiwia.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, alisema mfumo huo unaenda kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa mikopo pamoja na kuwajengea wadau uelewa mpana kuhusu shughuli zote za bodi.
Profesa Mushi aliongeza kuwa matumizi ya mfumo huo yatapunguza gharama za utoaji wa huduma za mikopo kwa takribani asilimia 60, jambo litakaloongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma.
Aidha, alitoa wito kwa wazazi na walezi kujifunza na kutumia mfumo huo mpya ili kupata taarifa sahihi kwa wakati, huku akisisitiza umuhimu wa mfumo kuwa na usalama wa taarifa (siri) na kutobagua, ili hata watu wenye mahitaji maalum waweze kuutumia bila changamoto.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Jackline Humbaro, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema amefurahishwa na huduma hiyo mpya kwani itawasaidia wanafunzi kuondokana na usumbufu wa kufanya safari za mara kwa mara kufuata huduma za mikopo.
Uzinduzi wa mfumo wa Bwana Bumu na Bibi Bumu unatajwa kuwa wa kipekee na wa kihistoria katika mageuzi ya utoaji wa huduma kwa wateja ndani ya sekta ya elimu nchini.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)




0 Comments