.Dar es Salaam.
Meneja wa TARURA Mkoa Shinyanga Mhandisi Avith Theodory amesema kuwa ndani siku 100 tangu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aingie madarakani katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita miradi 10 ya ujenzi wa barabara imesainiwa na tayari Wakandarasi wapo maeneo ya kazi 'site' wakiendelea na utekelezaji.
Hayo ameyasema pembezoni mwa Mkutano wa Mwaka wa Barabara uliondaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA) unaondelea kufanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jijini Dar es Salaam.
Amesema mikataba hiyo ya ujenzi pamoja na mambo mengine inahusu kurudisha mawasiliano yaliyokatika hasa maeneo ya vijijini kutokana na athari za mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2025/26.
Kwa mujibu wa Mhandisi Theodory mikataba hiyo pia inahusu ujenzi wa makalavati pamoja na madaraja makubwa mawili na kuongeza kuwa miradi hiyo ina faida kubwa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji mkoani humo.
"Kama nilivyosema baadhi ya barabara hizo zinazojengwa zilikuwa zimeathiriwa na mvua za mwaka 2025/26 kwa hiyo wananchi walikuwa hawawezi kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda katika masoko"
"Kukamilika kwa miradi hiyo itarahisisha wananchi hao kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda katika masoko hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Mkoa huu". Amefafanua.
Mhandisi Theodory ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuwa na utamaduni wa kuitunza miundombinu ya barabara kwa kuepuka kutupa takataka katika mitaro, kufanya shughuli za kibinaadamu pembezoni mwa barabara na kupitisha mifugo katika barabara ili kuepusha uharibifu wa barabara unaoweza kutokea.
Akizungumza ongezeko la bajeti katika Mkoa huo ndani ya miaka minne ambapo imepanda kutoka bilioni 6.4 hadi bilioni 18 Mhandisi Theodory amebainisha kuwa ongezeko hilo limewawezesha kufanya mambo makubwa mkoani humo ikwemo kufungua barabara mpya zaidi ya Km. 240, zaidi ya Km. 820 za barabara zimechongwa, na kuongeza mtandao wa barabara za lami kutoka Km 36 hadi kufikia zaidi ya Km. 42.






0 Comments