Header Ads Widget

KAMISHNA KUJI AFANYA ZIARA YA KIKAZI HIFADHI YA TAIFA ARUSHA


Na Philipo Hassan - Hifadhi ya Taifa Arusha 


Kamishna wa Uhifadhi  TANAPA, Musa Nassoro Kuji leo Januari 28, 2026 amefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Arusha na kuwasisitiza Maafisa na Askari Uhifadhi waliopo katika hifadhi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutunza maliasili zilizopo katika Hifadhi za Taifa.

Ziara ya Kamishna Kuji ililenga kufanya ukaguzi wa shughuli za uhifadhi na utalii pamoja na miundombinu inayotumiwa na watalii ambapo katika ukaguzi huo alifika maeneo mbalimbali  pamoja na maporomoko ya maji maarufu ya Tululusia.

Naye, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Steria Ndaga alimkaribisha Kamishna Kuji na kueleza maendeleo ya utekelezaji ya majukumu ya uhifadhi na utalii katika Hifadhi ya Taifa Arusha. 

Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji


Kamishna Ndaga alieleza kuwa “Tunaendelea kuboresha huduma kwa watalii pamoja na kuimarisha miundombinu inayotumiwa na watalii ambayo ni  pamoja na barabara, kambi za kulala watalii, na maeneo ya vivutio vya utalii”.

Aidha, Afisa Uhifadhi Mkuu Winfrida Misanga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Arusha alimshukuru Kamishna Kuji pamoja na Menejimenti ya Shirika kwa ujumla kwa kufanya ukaguzi katika hifadhi hiyo. Pia Misanga aliahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ili kuendeleza uboreshaji wa huduma kwa watalii wanaotembelea hifadhi.

Katika ziara hiyo, Kamishna Kuji  aliambatana na viongozi wengine wa Shirika akiwemo Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Massana Mwishawa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Izumbe Msindai - Mkuu wa Kanda ya Magharibi,

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meing’ataki - Mkuu wa Kanda ya Kusini na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi John Nyamhanga - Mkuu wa Kanda ya Mashariki.










Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI