Dar es Salaam
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA imeshiriki mkutano wa mwaka wa barabara uliondaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA).
Mkutano huo wa siku nne uliofunguliwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega umefanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Ujenzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Ulega amesema kuwa maboresho ya Sekta ya usafirishaji Tanzania inabaki kuwa ni kipaumbele cha Serikali na ni maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Serikali inaendelea kuwekeza katika upanuzi, maboresho na matengenezo katika mtandao wa barabara za Mijini na Vijijini kwa kutoa fedha katika matengenezo hayo, kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, ustahamilivu wa mabadiliko ya tabianchi, uendelevu wa mazingira katika maendeleo ya Miundombinu nchini." amebainisha Mhe. Ulega
Akiongea na Waandishi wa Habari pembezoni mwa mkutano huo Mhandisi Mshauri Pharles Ngeleja ambaye ni Mratibu wa ujenzi wa madaraja na barabara za mawe kutoka TARURA Makao Makuu amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Wakala mwaka 2017 mpaka Sasa Wakala huo umejenga madaraja ya mawe takribani 490 kwa gharama ya shilingi bilioni 40.
Kwa mujibu wa Mhandisi Ngeleja kama Madaraja hayo yangejengwa kwa kitumia njia ya zege na nondo Wakala ungetumia zaidi ya shilingi bilioni 140.
Mhandisi Ngeleja amesema kuwa kwa ujumla ili waweze kuifungua nchi wao kama Wakala wamewaomba washikadau wenzao ambao wanahusika na ujenzi wa miundombinu ya barabara kufanya ubunifu kwa kujenga barabara kwa kitumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo husika.
Mkutano huo kwa Mwaka huu umewakutanisha pia Wadau wa sekta ya ujenzi kutoka nchi za Senegal, Uganda, Namibia, Ghana, Guyana na Ujumbe kutoka Chama cha Barabara Duniani na ulibeba kaulimbiu isemayo "Mabadiliko ya Sekta ya Usafiri Barani Afrika: Kuimarisha, ufanisi, Ushirikiano na Uendelevu"










0 Comments