Header Ads Widget

KAIMU MKURUGENZI MKUU WA JAB ASIFU UWEKEZAJI WA MATUKIO DAIMA MEDIA



Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB, Wakili Patrick Kipangula (Katikati) akiwa na mkurugenzi wa Matukio Daima Media Mwanahabari Francis Godwin baada ya kutembelea  studio ya Matukio Daima Media mjini Iringa  leo kulia ni afisa habari wa JAB Editha Mayemba picha na Matukio Daima Media
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB, Wakili Patrick Kipangula (Katikati) akiwa na mkurugenzi wa Matukio Daima Media Mwanahabari Francis Godwin baada ya kutembelea  studio ya Matukio Daima Media mjini Iringa leo  kushoto ni afisa habari wa JAB Editha Mayemba picha na Matukio Daima Media


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB, Wakili Patrick Kipangula (wa sita kushoto) akiwa na mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Iringa (IPC) Frank Leonard (katikati) katibu wa IPC Hakim Mwafongo (wa nne kushoto) na baadhi ya waandishi mkoa wa Iringa  wa pili kulia afisa habari wa JAB Editha Mayemba


NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, ameusifu uwekezaji na kazi kubwa inayofanywa na Matukio Daima Media katika tasnia ya habari, akisema ni mfano mzuri wa vyombo vya habari vinavyozingatia misingi ya kitaaluma na maadili ya uandishi wa habari.

Wakili Kipangula, akiongozana na Afisa Habari wa JAB, Editha Mayemba, alitembelea studio za Matukio Daima Media zilizopo katika jengo la IMUCU katikati ya Manispaa ya Iringa. 

Katika ziara hiyo, alishuhudia maandalizi pamoja na mchakato wa uchakataji wa habari, na kueleza kuridhishwa kwake na mazingira ya kazi pamoja na juhudi zinazofanywa na chombo hicho katika kuhakikisha habari zinawasilishwa kwa weledi na kuzingatia sheria.

Kabla ya ziara hiyo, Wakili Kipangula alikutana na waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa katika ofisi zao na kuwakumbusha waandishi wote wasio na vitambulisho halali vya JAB kuacha mara moja kufanya kazi ya uandishi wa habari.

 Alisisitiza kuwa JAB imejipanga kikamilifu kusimamia taaluma ya habari nchini na haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu au chombo chochote kitakachokiuka taratibu zilizowekwa.

Akiwa Matukio Daima Media, Wakili Kipangula alieleza kuwa dhamira ya JAB si kuwatisha waandishi, bali kuwalea na kuwajengea uwezo kwa misingi ya kitaaluma. 

Alisema bodi itaendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwawezesha waandishi kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, sheria na weledi unaotakiwa.

Aliongeza kuwa waandishi wenye vyeti vya uandishi wa habari wanaoendelea na masomo ya Diploma hawataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi hadi watakapohitimu masomo yao. 

Hata hivyo, alibainisha kuwa wakati wa mafunzo kwa vitendo, waandishi hao wanaweza kuomba vitambulisho vya muda vya miezi mitatu kupitia mfumo wa Tai Habari, ambavyo vitapaswa kurejeshwa baada ya kukamilika kwa mafunzo.

Akizungumzia maboresho ya vitambulisho vya JAB, Wakili Kipangula alisema bodi inaendelea kuviboresha ili viweze kusomana na mifumo mingine ya serikali, ikiwemo NIDA, TRA na taasisi nyingine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matukio Daima Media, Francis Godwin, aliishukuru JAB kwa ziara hiyo na kupongeza kasi ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, akisema ameanza vizuri na ameonesha dhamira ya kuwasaidia vijana wanaoendesha mitandao ya kijamii kupata mitaji. 

Alisema Matukio Daima Media imefanikiwa kuwa na waandishi waliothibitishwa na JAB, huku changamoto kubwa ikiendelea kuwa hali duni ya kiuchumi katika uendeshaji wa chombo hicho.

Aliongeza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya JAB, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wadau wengine wa habari unaweza kuisukuma tasnia ya habari nchini kufikia hatua kubwa zaidi. 

Naye Mwenyekiti wa IPC, Frank Leonard, aliipongeza JAB kwa jitihada zake za kusimamia misingi ya kitaaluma na kuahidi kuendelea kushirikiana na bodi hiyo katika kukuza na kuimarisha taaluma ya habari nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI