NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,MOROGORO Watu 10 wameripotiwa kufariki na wengine 18 kujeruhiwa sehemu mbalimbali ya miili yao katika tukio la ajali ya kuteketea moto kwa magari baada ya kugongana uso kwa uso katika Kijiji cha Maseyu Kata ya Gwata Wilaya ya Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku kwa waandishi wa habari mkoani Morogoro na Kamanda wa Polisi mkoani humo SACP Alex Mkama, amesema tukio hilo limetokea Disemba 31 majira ya jioni likihusisha magari mawili ambapo gari T 162 DMD aina ya Mitsubish Fuso likiendeshwa na Dereva Swalehe Juma Adamz liligongana na gari la mizigo lenye namba za usajili T 828 ELW aina ya Carry trailer lilokuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Abuu mkazi wa Msoga-Chalinze akitokea Dar es salaam kuelekea Mbeya akiwa na shehena ya mbolea.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa miili ya watu 10 waliofariki katika ajali hiyo bado haijatambuliwa kwa majina na jinsi zao kutokana na kuungua vibaya, ambapo majeruhi 18 waliofikishwa kwa ajili ya matibabu wanaume 9 na wanawake 9 ambapo kati yao ni watoto 05 wakike wawili na wakiume watatu huku abiria 06 wakipata mivunjiko sehemu mbalimbali.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi umeibani, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la mizigo kuhamia upande wa kulia zaidi alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kisha kugongana uso kwa uso na kuwaka moto.
Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusisna na tukio hilo likihusisha pia utambuzi wa miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo, huku likitoa wito kwa madereva wote kuheshimu sheria za usalama barabarani pamoja na kuchukua tahadhari kubwa kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ili kuokoa maisha ya watu na mali.






0 Comments