Header Ads Widget

VIJANA WAACHE KUTEGEMEA AJIRA SERIKARINI,WAANZE KUJIAJIRI


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais  Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema tatizo la ajira kwa vijana nchini linachochewa na mtazamo wa kutegemea ajira serikalini, akibainisha kuwa fikra hizo ‘zimepitwa na wakati’ katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Prof. Mkumbo alisema zama za mhitimu kupata ajira serikalini mara tu baada ya kuhitimu chuo zimekwisha, na Serikali inaelekeza nguvu katika kujenga uwezo wa vijana kujiajiri, kuwekeza na hatimaye kuajiri wenzao.

Amesema changamoto hiyo haipo Tanzania pekee, bali inagusa mataifa mengi barani Afrika, ambapo nafasi za ajira serikalini hazikidhi idadi kubwa ya wahitimu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. “Serikali haiwezi kubaki kuwa mwajiri mkuu wakati uwezo wake wa kuajiri ni mdogo ukilinganisha na mahitaji. Suluhisho ni kupanua sekta binafsi na kuwawezesha vijana kuwa injini ya ajira,” amesema.

Katika kupanua fursa hizo, Serikali inakwenda kuanzisha Kituo Maalum cha Kuhudumia na Kuwezesha Wawekezaji Vijana (Youth Investors Resource Centre) kitakachotoa mafunzo, ushauri na huduma mbalimbali kwa vijana wenye nia ya kuwekeza. Kituo hicho kitakuwa Mabibo, Dar es Salaam, na kitakuwa na uwakilishi katika ofisi za TISEZA za mikoa na kanda. Waziri alisema anatarajia kukizindua kituo hicho kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Aidha, Serikali inaanzisha programu maalum ya kuwawezesha vijana kuanzisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo mbalimbali nchini. Kupitia mpango huo, maeneo mahsusi yametengwa kwa wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi ili kuwasaidia kuanzisha miradi ya viwanda na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI