Serikali imeweka kipaumbele katika kuhuisha majengo na kupanga upya miji mikubwa nchini, hatua inayolenga kuongeza thamani ya makazi, kuboresha matumizi ya ardhi na kuvutia uwekezaji katika kipindi cha pili cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema mpango huo utafanyika kwa ubia kati ya wananchi na sekta binafsi kwa kubomoa nyumba chakavu na kujenga majengo mapya ya ghorofa. Wakazi waliopo katika maeneo husika watapewa sehemu za makazi na biashara katika majengo mapya kama sehemu ya uwezeshaji na kunufaika na mradi.
Akitaja maeneo yatakayoanza kutekelezewa mpango huo, Prof. Mkumbo alisema Serikali imeshatenga Vingunguti, Buguruni na Manzese jijini Dar es Salaam, na taratibu za kuwavutia wawekezaji zitatangazwa muda mfupi ujao. Alisisitiza kuwa wakazi hawatapoteza haki zao, kwani watahakikishiwa kupata ‘floors’ za makazi na biashara pindi majengo mapya yatakapokamilika.
Waziri huyo amesema kuwa mageuzi ya miji ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali kufungua fursa za kiuchumi, kuongeza ajira na kuboresha ubora wa maisha hasa katika maeneo ya mijini. Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Dar es Salaam na baadaye miji mingine inakuwa na makazi yaliyopangwa kisasa na miundombinu bora.
Katika hatua nyingine, Prof. Mkumbo alisema Serikali inaongeza juhudi katika kufungua maeneo mapya ya utalii nje ya ukanda unaotembelewa zaidi wa Kaskazini. Alitaja Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kama eneo lenye uzuri wa kipekee ambalo bado halijatumika ipasavyo, sambamba na fukwe nyingi za Tanzania ambazo hazijawekewa mkazo wa kutosha licha ya nchi kuwa na mwambao mrefu wenye vivutio vingi.
Alibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwekezaji katika utalii, ujenzi na miundombinu, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza mapato ya taifa na kupanua ajira kwa vijana.







0 Comments