Katika kuendeleza juhudi za kulinda afya ya jamii, Meneja wa TMDA Kanda ya Kusini, Dkt. Engelbert B. Mbekenga, ameongoza timu ya wataalamu wa mamlaka hiyo katika kampeni maalum ya kutoa elimu kwa watumishi wa sekta ya afya na wananchi kuhusu njia sahihi za kutoa taarifa za madhara yanayoweza kusababishwa na dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na chanjo.
Zoezi hilo limefanyika katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya kusini likiwa na lengo la kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa sahihi kuhusu umuhimu wa kutuma taarifa za matukio hayo.
Dkt. Mbekenga ameeleza kuwa TMDA Kanda ya Kusini imejikita kuwafikia wahudumu wa afya katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, sambamba na jamii kwa ujumla, ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kuripoti madhara yanayotokana na matumizi ya bidhaa za afya.
Amesema, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuboresha usalama wa matumizi ya bidhaa hizo kwa wananchi.
Katika mafunzo hayo, TMDA imeeleza kuwa zipo njia nne kuu ambazo watumishi wa sekta ya afya na wananchi wanaweza kutumia kuripoti madhara.
Njia ya kwanza ni kujaza fomu maalum zinazopatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya. Njia ya pili ni kupiga simu bure 0800 110 084 bila kukatwa salio. Tatu ni kutumia 15200# kisha kuchagua sekta ya afya na kutuma taarifa. Njia ya nne ni kupitia mfumo wa SQRT ambapo mtu hupata fomu ya kidijitali, kuijaza na kuituma moja kwa moja.
Kampeni hii ya elimu imeendelea kutekelezwa katika Halmashauri za Masasi Mji, Wilaya ya Masasi, Newala Mji na Wilaya ya Newala.
Zoezi lilianza rasmi tarehe 23 Novemba 2025 na linatarajiwa kukamilika tarehe 5 Desemba 2025. TMDA Kanda ya Kusini inalenga kuwafikia watumishi wote wa hospitali, vituo vya afya, zahanati pamoja na wananchi katika maeneo hayo ili kuhakikisha taarifa za matukio ya madhara zinatumwa kwa usahihi na kwa wakati.
Dkt. Mbekenga amebainisha kuwa utoaji wa elimu unalenga kuongeza mwitikio wa utoaji taarifa kutoka kwa watumishi wa afya na jamii, kwani taarifa hizo ni muhimu katika kuboresha matumizi salama ya dawa na vifaa tiba. Kwa mujibu wake, uelewa mdogo umekuwa moja ya changamoto kubwa inayosababisha wananchi kutoripoti madhara wanayokutana nayo baada ya kutumia bidhaa za afya.
Elimu hiyo pia imewafikia akina mama wanaoleta watoto kupata chanjo mbalimbali, pamoja na wananchi wanaotumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs).
TMDA imebainisha kuwa kundi hili limekuwa likikumbana na baadhi ya madhara lakini wengi wao hawajui kuwa dalili fulani zinazoonekana baada ya kutumia dawa au chanjo zinaweza kuwa madhara yanayohitaji kuripotiwa.









0 Comments