Na Moses Ng’wat, Ileje.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, wamempitisha kwa kishindo Diwani wa Kata ya Chitete, Osiwelo Chomo, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri baada ya kupata kura zote 24.
Uchaguzi huo umefanyika kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Desemba 4, 2025 na kusimamiwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje (DAS), Abdallah Mayomba.
Katika uchaguzi huo, Diwani wa Kata ya Sange, Hakika Kajange, naye alipata kura zote 24 na kutangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ambapo wagombea wote wawili hawakuwa na wapinzani.
Akitangaza matokeo hayo, Mayomba aliwataka viongozi hao kuonesha ushirikiano, uwajibikaji na kuongeza kasi katika kusimamia miradi ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kipindi chote cha uongozi wao wa miaka mitano.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa, Chomo aliahidi kufanya kazi kwa karibu na madiwani, wataalamu na wananchi ili kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha sekta ya kilimo ambayo ni msingi wa uchumi wa wananchi wa Ileje, akizitaka kamati husika kushirikiana na wataalamu kutatua changamoto zinazokwamisha uzalishaji.









0 Comments