Header Ads Widget

SENYAMULE:TUIMARISHE MAOMBI NA KULINDA AMANI KUELEKEA DESEMBA 9

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa dini kuhakikisha maombi yanawekwa mbele na kila mmoja anatimiza wajibu wake katika kulinda amani ya nchi, hasa katika kipindi hiki ambacho zimekuwepo taarifa za uwezekano wa machafuko kuelekea Desemba 9.

“Kila mmoja ana wajibu wa kulinda amani wakati huu si wa kusubiri tu tarehe 9 itakuwaje hatupaswi kulala leo ili kuhakikisha kesho kunakuwa na salama,” amesema Senyamule akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kuchukua hatua.

Ameongeza kuwa viongozi wa dini wana nafasi ya kipekee katika kuhamasisha umoja, maelewano na kutuliza mioyo ya wananchi, hasa kipindi hiki ambacho kumekuwa na taharuki katika maeneo mbalimbali.

“Huu si wakati wa kulala usingizi huu ni wakati wa kushikana na kuzungumza lugha ya amani tukifanya hivyo, tutakuwa tumetimiza wajibu wetu,” amesema.

Akizungumza leo wakati wa kufungua kikao maalumu cha maombi kilichowakutanisha viongozi wa dini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Senyamule alisema Serikali imeweka siku tatu Desemba 7, 8 na 9 kuwa za maombi ya kuombea utulivu na mshikamano wa taifa.


Mkuu huyo wa Mkoa pia aliwataka wananchi kuendelea kumuomba Mungu ili Tanzania ibaki kuwa nchi ya utulivu, upendo na mshikamano.

Kikao hicho cha maombi kilihudhuriwa na viongozi kutoka madhehebu mbalimbali, ambao walitumia nafasi hiyo kuiombea nchi na kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani.

Wakati wa kufunga maombi hayo, Senyamule amesisitiza kuwa kuna watu wachache wanaotamani uvunjifu wa amani, hivyo wananchi wanaopenda amani wanapaswa kuendelea kupaza sauti na kuonesha umoja katika kipindi hiki cha siku tatu za maombi.

“Tusilale tuendelee kupaza sauti, tufanye wajibu wetu wa kidini, na kubwa zaidi tuungane kuhakikisha amani inaendelea kutawala,” amesema.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI