Na Moses Ng'wat, Mbozi.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, wamekumbushwa kuviishi viapo vyao, ikiwamo ahadi ya Uadilifu, kwa kusimamia majukumu yao bila kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha mgongano wa maslahi, ambavyo vimetajwa kuwa chanzo cha kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rai hiyo ilitolewa Novemba 5, 2025 na Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Majid Mohamed, wakati madiwani hao wakiahidi kutekeleza kiapo chao mara baada ya kuapishwa katika mkutano wa kwanza wa baraza hilo.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Vwawa Day, wilayani humo, na ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na watendaji wa Halmashauri, wakiwemo wananchi kutoka kata mbalimbali.
Mohamed alisema madiwani hawapaswi kushiriki au kujihusisha kwa namna yoyote na zabuni zinazotangazwa na Halmashauri, kwani kufanya hivyo kunahatarisha uwazi na haki .
Aidha, aliwakumbusha kuwa zawadi wanazopokea baada ya kuwahudumia wananchi hazipaswi kuzidi kiasi cha shilingi 200,000, na endapo zitazidi kiwango hicho wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi ili ziwekwe kwenye mpango rasmi wa matumizi.
Baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la kiapo, Madiwani wa Halmashauri hiyo, wamemchagua kwa kishindo Diwani wa Kata ya Halungu, Maarifa Mwashitete, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, akiibuka na kura zote 40.
Baraza hilo lilitarajiwa kuwa na madiwani 41, lakini idadi hiyo ilipungua kufuatia kifo cha diwani mteule wa Kata ya Shiwinga aliyefariki dunia siku chache kabla ya kuapishwa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kunywa maji ya betri.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi, Mbwana Kambangwa, alimtangaza pia diwani wa viti maalum, Fausta Kibona kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, naye akijizolea kura zote 40.
Akizungumza mara baada ya kufungua kikao cha kwanza cha baraza hilo, Mwashitete, alishukuru baraza la madiwani kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwaongoza, huku akiahidi kusimamia kwa nguvu zote kasi ya ukusanyaji wa mapato inayoendana na matumizi sahihi ya fedha hizo zilizokusanywa.
Aidha, alisema hatavumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ya ukusanyaji mapato.
Akitumia nafasi hiyo kutoa salam za serikali, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amewataka madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi kama timu moja ili kuisukuma mbele Halmashauri ya Mbozi. Mbega amesisitiza umuhimu wa madiwani kutanguliza maslahi ya wananchi na kutunza siri za vikao, sanjari na kujiepusha na vitendo vinavyowavunjia heshima kama matumizi ya lugha chafu na ulevi.



.jpeg)
.jpeg)




0 Comments