Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa Kila Mwananchi kuendelea kutii sheria sambamba na kushirikiana na kila mmoja kwa nafasi yake katika kulinda na kuimarisha amani, hasa kwa kuzingatia umuhimu wa amani katika maisha na shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi.
Polisi pia kupitia kwa Msemaji wake David Misime, limesisitiza kuendelea kuelimishana na kuhimizana katika kuyakataa yale yote yanayohamasishwa kwa njia mbalimbali ili kuwachonganisha na kuwajengea chuki Watanzania, lengo likiwa ni kuwaingiza Watanzania katika vurugu ambazo mara zote zimekuwa si nzuri kulingana na kile kinachoshuhudiwa kwenye Mataifa mengine duniani.
"Jeshi la Polisi pia kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama vinaendelea kuwaahidi kuwa tutaendelea kulinda usalama wa nchi yetu sote, maisha na mali za kila mmoja ndani ya Taifa letu la Tanzania." Amesema Msemaji huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime.
Katika hatua nyingine, Polisi imeeleza kuwa nchi bado ni salama na shughuli za kiuchumi na za kijamii zinaendelea vyema katika kipindi cha saa 24 zilizopita, likishukuru pia kwa ushirikiano wanaoendelea kuupata kutoka kwa wananchi wa Tanzania.






0 Comments