Header Ads Widget

WFP -FtMA WAWEZESHA MAFUNZO KWA WAZALISHAJI 50 WA MBEGU ZA KUAZIMIWA UBORA NJOMBE,IRINGA NA MBEYA



Jumla ya wazalishaji 50 wa mbegu za kuazimiwa ubora (UMBEGU) wamepatiwa mafunzo maalum ya siku mbili yanayolenga kuongeza ujuzi na uwezo wao katika uzalishaji wa mbegu bora za maharage na mpunga. 

Mafunzo hayo yanafanyika katika mji wa Makambako mkoani Njombe, yakitolewa na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI) chini ya ufadhili wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kupitia mpango wa Farm to Market Alliance (FtMA).


Washiriki wa mafunzo hayo wanatoka katika maeneo mbalimbali ya kanda ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo wilaya za Kilolo, Mufindi, Wanging’ombe, Njombe, Iringa, Mbarali na Mbeya DC. 

Ushiriki wa wakulima kutoka maeneo tofauti unaonesha umuhimu wa mafunzo haya katika kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora katika ukanda unaotegemewa kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.


Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwezesha vituo vya watoa huduma kwa wakulima, hususan wazalishaji wa mbegu za kuazimiwa ubora, kuzalisha mbegu zenye viwango vinavyokubalika kitaifa, zenye ubora wa hali ya juu, upatikanaji rahisi na bei nafuu kwa wakulima wadogo. Kupitia mpango huu, wakulima wanatarajiwa kunufaika kwa kupata mbegu bora karibu na maeneo yao, hivyo kuongeza uzalishaji na tija katika mashamba yao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mratibu wa FtMA–Nafaka Kilimo Iringa, Moses Logan, alisema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa juhudi za FtMA–Nafaka Kilimo Iringa katika kuwajengea uwezo wakulima na wadau wa sekta ya kilimo.

 Alieleza kuwa mpango wa FtMA umejikita katika kuunganisha wakulima na masoko, pembejeo na maarifa ya kisasa ili kuboresha mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo.


“Mafunzo haya ya siku mbili yanayofanyika hapa Makambako ni sehemu ya mkakati mpana wa FtMA wa kuwawezesha wakulima na wazalishaji wa mbegu kuwa na uelewa wa kina kuhusu uzalishaji wa mbegu bora. Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kuona ongezeko la uzalishaji wa mbegu bora za maharage na mpunga zitakazosaidia wakulima wengi zaidi,” alisema Logan.

Kwa upande wake, mtaalamu kutoka TOSCI Laurent Mfagavo ambae ni mkaguzi wa Mbegu alieleza kuwa mafunzo yanahusisha masuala muhimu ya kiufundi ikiwemo taratibu za usajili na uthibitishaji wa mbegu za kuazimiwa ubora, uchaguzi wa mashamba yanayofaa kwa uzalishaji wa mbegu, udhibiti wa magonjwa na wadudu, pamoja na namna ya kuvuna, kuhifadhi na kusambaza mbegu bila kupunguza ubora wake. 


Alisisitiza kuwa kufuata kanuni na viwango vilivyowekwa ni jambo la msingi katika kuhakikisha mbegu zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaoaminika na wakulima.


Baadhi ya washiriki walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa matumaini mapya katika shughuli zao za kilimo. Mkulima wa mpunga, Oscar Joseph Budu kutoka Kijiji cha Manienga, Wilaya ya Mbarali, alisema kuwa mafunzo hayo yatamwezesha kuzalisha mbegu bora na kuwauzia wakulima wengine katika eneo lake.


 “Kupitia mafunzo haya nimejifunza mbinu bora za uzalishaji wa mbegu za mpunga. elimu hii itanisaidia sio tu kuongeza kipato changu, bali pia kuwasaidia wakulima wenzangu kupata mbegu bora kwa urahisi,” alisema Budu.


Mkulima wa maharage, Veronica Lukenda kutoka Kijiji cha Manga, Wilaya ya Wanging’ombe, alisema kuwa kwa mara ya kwanza amepata fursa ya kushiriki mafunzo ya aina hiyo. 

Alieleza kuwa awali alikuwa akilima maharage bila ujuzi wa kitaalamu kuhusu uzalishaji wa mbegu bora “Sijawahi kupata mafunzo kama haya hapo awali Leo ni fursa kubwa kwangu kupata ujuzi utakaonisaidia kuongeza uzalishaji, kipato na kuchangia kukuza uchumi wa familia yangu,” alisema Veronica.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo kwa wakulima na wazalishaji wa mbegu katika maeneo husika, kwa kuwa yataongeza upatikanaji wa mbegu bora zinazozalishwa ndani ya jamii.

 Hali hii itapunguza gharama za mbegu, kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao na kuchangia katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe.


Kwa ujumla, mafunzo ya wazalishaji wa mbegu za kuazimiwa ubora yanayofanyika Makambako yanaonesha ushirikiano mzuri kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na wakulima katika kuendeleza sekta ya kilimo. 


Kupitia uwekezaji katika elimu na ujuzi wa wakulima, Tanzania inaendelea kuchukua hatua muhimu kuelekea kilimo chenye tija, chenye ushindani na chenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI