Header Ads Widget

MALAWI YAFUNGUA FURSA KWA WATANZANIA,WAFANYA BIASHARA WAITWA

Na Moses Ng’wat, Ileje.

BALOZI wa Tanzania nchini Malawi, Agnes Kayola, amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana Malawi, hususan katika sekta za kilimo, usafirishaji na utalii.

Akizungumza Novemba 2, 2025, wakati wa ziara yake ya siku moja katika kituo cha forodha Isongole, Wilaya ya Ileje, Balozi Kayola alisema Malawi inahitaji kwa kiwango kikubwa mahindi kutokana na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hali iliyoongeza mahitaji ya bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi hiyo.

“Zipo fursa nyingi. Kuanzia biashara ya mahindi, hoteli, utalii, mpaka biashara ndogo kama migahawa na vituo vya kuosha magari (Car Wash) za kisasa hivyo watanzania mkijipanga mna nafasi nzuri ya kwenda kuwekeza,” alisema Balozi Kayola.

Aidha, alieleza kuwa serikali ya Malawi imefungua mlango kwa wawekezaji wa nje katika miradi ya ujenzi wa hoteli, utalii wa maji katika ukanda wa Ziwa Nyasa kwa upande wa Malawi, pamoja na usafiri wa anga, huku mazungumzo ya safari za ndege za ATCL kati ya Tanzania na nchi hiyo yakikaribia kukamilika.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Isongole, Wilayani Ileje, Edvine Mwakibasa, alisema kituo hicho kinaendelea kudhibiti uingizaji na utokaji wa mizigo mpakani, kukadiria na kukusanya kodi kwa mizigo midogo, pamoja na kuzuia magendo kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali za serikali.

Akitoa taarifa ya utendaji kwa robo ya kwanza (Julai–Novemba 2025), Mwakibasa alisema kituo kimekusanya Sh. 83,066,285, sawa na asilimia 30.21 ya lengo.

 

Awali, Balozi Kayola alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, na kufanya mazungumzo kuhusu kuongeza mchango wa mkoa huo katika kukuza biashara na mahusiano kati ya Tanzania na Malawi.

Mazungumzo hayo yalijikita pia katika kuboresha mazingira ya mpakani na kuondoa changamoto zinazokwamisha shughuli za kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI