Matukio Daima, Morogoro
MKULIMA Rashid Hussein Paulo (35), mkazi wa Msowero wilayani Kilosa Mkoani Morogoro anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Steven Elia Mayungu (26), mkulima na mkazi wa Mayungu baada ya mgogoro unaodaiwa kuhusishwa na wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, tukio hilo limetokea Desemba 26, 2025 majira ya saa 5 usiku katika Kitongoji cha Shuleni, Kijiji na Kata ya Lumuma, Wilaya ya Kilosa.
Uchunguzi wa awali umeeleza kuwa mtuhumiwa anadaiwa kumchoma marehemu kwa kitu chenye ncha kali katika eneo la kifua baada ya ugomvi kutokea kati yao, ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimhisi marehemu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wake.
Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa yupo chini ya ulinzi wa Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku taratibu za kisheria zikiendelea.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo halali kutatua migogoro ya kifamilia ili kuepusha madhara makubwa kama hayo.
Mwisho






0 Comments