Meneja benki ya CRDB, Tawi la Maswa,Hezron Ikelesho (kulia) akimakabidhi Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano(kushoto)meza ikiwa ni sehemu ya meza 30 na viti 30 katika shule ya sekondari Nyongo.Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
KATIKA jitihada za kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya elimu nchini, Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa imekabidhi meza 30 na viti 30 katika Shule ya Sekondari Nyongo, wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Makabidhiano hayo yamefanyika jana katika shule ya sekondari Nyongo iliyopo kata ya Sola, kati ya Meneja wa CRDB tawi la Maswa, Hezron Ikelesho na Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Naano, aliishukuru CRDB kwa hatua hiyo amesema ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za fedha katika kuchangia maendeleo ya taifa.
“Tunapongeza CRDB kwa kuona umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu. Huu ni ushahidi kuwa maendeleo ya elimu si jukumu la Serikali peke yake bali ni wajibu wa wadau wote,” amesema.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Nyongo wakiwa wamekalia viti na meza zilizotolewa na benki ya Crdb tawi la Maswa.Dkt Naano pia amewataka wanafunzi na walimu kutunza samani hizo na kuhakikisha zinatumika kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Meneja wa CRDB tawi la Maswa, Hezron Ikelesho ambaye pia alimwakilisha Meneja wa Benki hiyo kanda ya Ziwa amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya miaka mitatu ijulikanayo kama “Keti Jifunze” inayolenga kuzisaidia shule nchini kupata samani bora za madarasa ili kuboresha elimu kwa vitendo.
“Tunataka kila mtoto wa Kitanzania asome kwenye mazingira rafiki, salama na yenye staha. ‘Keti Jifunze’ ni zaidi ya kampeni ni uwekezaji katika mustakabali wa taifa,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amesema kuwa msaada huo umekuja kwa muda muafaka kwani shule hiyo bado ni mpya na hivyo bado inahuhitaji mkubwa wa samani.
‘Msaada huu wa benki ya CRDB kwa shule yetu mpya ya Nyongo ni wa maana sana na tunatambua ya kuwa CRDB ni wadau muhimu sana wa maendeleo hapa nchini,sisi kama halmashauri ya wilaya ambao ndiyo wenye shule tumeupokea kwa mikono miwili,”amesema.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Maisha Budeba amesema walikuwa wakikaa wanafunzi wawili katika kiti kimoja jambo lililokuwa likisababisha usumbufu wakati wa kuandika.
“Tulikuwa tunaandika kwa kubanana sana, mara nyingine wengine tunasimama tukisubiri nafasi. Sasa tumeweza kukaa vizuri na kuandika bila shida. Tunashukuru sana CRDB,” amesema.
Naye Lugombela Mathias mwanafunzi wa kidato cha tatu, amesema meza na viti vipya vitawasaidia kuzingatia masomo kwa muda mrefu bila uchovu.
“Kabla tulikuwa tunakaa kwenye madawati yaliyoharibika, tulikuwa tunachoka mapema. Sasa tunajisikia vizuri kuwa kwenye darasa, tunasoma kwa utulivu,” amesema
Kwa upande wake, Sarah Edward, mwanafunzi wa kidato cha kwanza, amesema msaada huo umewapa matumaini mapya na kusukuma ndoto zao za baadaye.
“Tumeingia sekondari na sasa tuna mazingira mazuri. Inatupa nguvu ya kusoma kwa bidii ili tufikie malengo yetu,” amesema.
Ujenzi wa Shule ya Sekondari Nyongo, unaokadiriwa kugharimu zaidi ta Shilingi Milioni 400 umeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kupunguza adha ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu na kuongeza ufaulu kupitia miundombinu bora ya kujifunza.
MWISHO.
![]() |













0 Comments