Header Ads Widget

JESHI LA MAGEREZA LATEKELEZA AGIZO LA SERIKALI LA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA*



📌*Gharama nafuu yawa chachu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.*

📌*Wizara ya Nishati yawapongeza*

📍Simiyu

Jeshi la Magereza nchini limetekeleza agizo la Serikali la matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 suala linaloifanya jeshi hilo kujikinga na athari zinazotokana na  nishati isiyo safi ya kupikia kama vile kuni na mkaa.

Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi wa Ofisi za Magereza Mkoani Simiyu Bw. Simon Kotti , wakati wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia walipofanya ziara kwa lengo la kufuatilia miradi ya usambazaji wa Nishati Safi ya Kupikia na Teknolojia zake ikiwemo matumizi ya Rafiki Briquettes katika Magereza ili kubaini changamoto mbalimbali kama zipo.

Kamishna msaidizi ameeleza kuwa kwa kuzingatia maelekezo ya agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye taasisi zinazolisha watu zaidi ya mia moja wao kama magereza walishalitekeleza hilo ili kujikinga na athari za matumizi ya nishati isiyo safi na salama.


Kotti amesema “sisi kama Jeshi la Magereza tunaendelea kuhakikisha tunajikita katika matumizi ya nishati safi ambapo kwasasa tunatumia nishati mbadala ya makaa ya mawe ambayo kulingana na uhitaji wetu tunanunua kwa gharama ya shilingi laki nane ikiwa ni gharama pungufu na kuni ambapo gharama yake ilikuwa mara mbili ya makaa ya mawe” amesema Kotti.

Sambamba na hilo Kamishna msaidizi wa Magereza Mkoani Simiyu amesema kwa upande wa Magereza ya Wilaya ya Bariadi inaendelea na mradi wa kujenga gesi vunde kwa ajili ya kupikia ambapo  mradi huo upo katika hatua ya kukusanya vifaa vya ujenzi na utakapo kamilika utasaidia kuongeza chanzo kingine cha nishati safi na pia kuchangia katika utekelezaji wa  Mkakati wa wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Naye,  Mtaalam  kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Omari Khalifa amepongeza juhudi za Jeshi la Magereza nchini katika Utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku akikisistiza umuhimu wa kuendelea kutumia nishati safi  ili kujikinga na athari za kiafya na mabadiliko ya tabia  nchi.


Aidha Bw. Khalifa ametoa angalizo la  sehemu za kutunzia Mkaa wa Makaa ya mawe ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza endapo nishati hiyo haitotunzwa sehemu salama.

“Nasisitiza kuboresha sehemu za kutunzia Mkaa wa Makaa ya mawe, ili nishati hiyo isiweze kuathirika, kwani utunzaji mzuri utaendelea kusaidia kupata nishati iliyo bora zaidi na kwa kiwango kilichokusudiwa pasipo changamoto yoyote” amesema Bw. Khalifa.

Katika hatua nyingine Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati  wametembelea Gereza la Musoma lililopo Wilaya ya Musoma Mkoani Mara ili  kujionea miundombinu ya Nishati safi ya kupikia na jinsi nishati hizo zinavyotunzwa.

#NishatiTupokazini




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI