Header Ads Widget

SAMIA ARDHI KLINIKI YAWAVUTA WANAWAKE WENGI IRINGA

 


Na Easter Kameta (UoI),Matukio Daima Media 

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, wanawake wengi mkoani Iringa wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika huduma za Samia Ardhi Kliniki, kampeni inayolenga kutoa elimu na huduma mbalimbali zinazohusiana na umiliki wa ardhi.

Kliniki hiyo inaendelea katika viwanja vya Bustani ya Manispaa ya Iringa na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 7 mwaka huu, siku moja kabla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani. 

Kupitia huduma hiyo, wanawake waliokuwa hawana umiliki rasmi wa ardhi wanapatiwa fursa ya kupata hati halali za kumiliki ardhi pamoja na elimu ya kisheria kuhusu haki zao.

Mbali na utoaji wa hati, kliniki hiyo pia inalenga kuwajengea uwezo wanawake kuelewa sheria na sera zinazohusu ardhi ili waweze kutetea haki zao katika jamii.

 Huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa hasa kwa wanawake ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kimila na kijamii zinazowazuia kumiliki ardhi.

Akizungumza na Matukio Daima, Afisa Mteule wa Manispaa ya Iringa, Zera Chaula, alisema kuwa Samia Ardhi Kliniki ni mpango unaotekelezwa nchi nzima kwa lengo la kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapatia huduma zinazohusu ardhi pamoja na elimu ya sheria za umiliki wa ardhi.

Alieleza kuwa katika mkoa wa Iringa, kliniki hiyo imeunganisha halmashauri tano ambazo ni Manispaa ya Iringa, Kilolo, Mafinga, Mufindi na Iringa Vijijini. Kupitia mpango huo, wananchi wanapata fursa ya kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na ardhi bila kulazimika kufuata taratibu ndefu za kiofisi.

“Kwa kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani, serikali imeandaa kliniki maalumu inayohusiana na masuala ya ardhi. Lengo ni kutoa huduma mbalimbali za ardhi, kutoa elimu kuhusu sheria za umiliki wa ardhi kwa wanawake, kuhamasisha wanawake kujua sera ya ardhi pamoja na haki zao za kumiliki ardhi, na pia kutoa hati za umiliki kwa wale wanaokidhi vigezo,” alisema Chaula.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Iringa, Catheline Charwe, alisema kuwa kampeni hiyo imeleta manufaa makubwa kwa wanawake katika jamii, hasa katika kutatua migogoro ya mirathi ambayo imekuwa ikiwanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi.

Alisema kupitia kliniki hiyo, pande zinazohusika katika migogoro ya mirathi zimepewa elimu kuhusu sheria za mirathi na haki za wanawake, jambo ambalo limechangia kupunguza migogoro na kuimarisha usawa katika jamii.

“Wanawake wengi wameanza kukombolewa kupitia Samia Ardhi Kliniki kwa kupata hati zao kwa kuzingatia sheria. Pia tumefanikiwa kutatua baadhi ya migogoro ya mirathi kwa kutoa elimu kwa pande zote mbili na kuhimiza jamii kupinga mfumo dume unaowanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi,” alisema Charwe.

Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Iringa, Frola Shija, alisema kampeni hiyo imelenga kumuwezesha mwanamke kiuchumi kwa kumpatia haki ya kumiliki ardhi.

Alifafanua kuwa hadi sasa wanawake kati ya 150 hadi 250 katika mkoa wa Iringa tayari wamefanikiwa kupata hati zao papo kwa papo kupitia kliniki hiyo. 

Hata hivyo alisisitiza kuwa huduma hizo hazikulenga wanawake pekee, bali zinawahusu wananchi wote wakiwemo wanaume.

“Kampeni hii ni kwa ajili ya watu wote, wanawake na wanaume. Hata hivyo, mwitikio mkubwa hapa Iringa umetoka kwa wanawake hii inaonyesha jinsi wanawake walivyokuwa na uhitaji mkubwa wa kupata haki zao za kumiliki ardhi,” alisema Shija.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo pia imechangia kuboresha uelewa wa jamii kuhusu haki za wanawake na kupambana na mila na desturi zinazowakandamiza wanawake katika suala la umiliki wa mali.

Mkazi wa Mawelewele mkoani Iringa, Aisha Said, alisema kuwa Samia Ardhi Kliniki imekuwa msaada mkubwa kwa wanawake katika jamii, kwani imewapa fursa ya kupata haki zao ambazo kwa muda mrefu zilikuwa zikinyimwa kutokana na mila na desturi.

“Kliniki hii imekuwa msaada mkubwa kwetu kwa sababu wanawake wengi walikuwa wakinyanyasika katika suala la umiliki wa ardhi kupitia mfumo huu, sasa wanawake wanaweza kumiliki ardhi na pia tumepatiwa hati zilizothibitishwa kisheria,” alisema Aisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi, amepongeza huduma hiyo akisema imekuwa chachu ya kumkomboa mwanamke na kumwezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kamishina msaidizi wa Ardhi mkoa wa Iringa Rehema Kilonzi alisema kuwa wiki ya Samia Ardhi Kliniki imekuwa na matokeo makubwa kwani toka wanze tayari hati 127 zimekwisha tolewa hadi Machi 4 mwaka huu.

Kuwa hati hizo zinakwenda kubadilisha mtazamo katika jamii uliokuwa ukiwatenga wanawake nchini ila kwa sasa wanawake wanakwenda kumiliki Ardhi kwa kuwa na hati zao .

Alisema kuwa huduma hiyo imekuwa ni msaada mkubwa kwa wanawake nchini na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuja na huduma hiyo nzuri ambayo inaendana na dira ya Taifa 2050.

Alisema umiliki wa ardhi kwa wanawake ni jambo muhimu katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza uwezo wa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Kwa mujibu wa sera ya ardhi ya Tanzania, wanawake wana haki sawa na wanaume katika kumiliki ardhi na mali nyingine. Hata hivyo, changamoto za kimila na kijamii zimekuwa zikikwamisha utekelezaji wa haki hizo katika baadhi ya maeneo.

Katika muktadha huo, juhudi za serikali kupitia kampeni kama Samia Ardhi Kliniki zinaonekana kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha wanawake wanapata haki zao za msingi, ikiwemo umiliki wa ardhi.

Aidha, suala la uwezeshaji wa wanawake linatajwa pia katika mipango ya maendeleo ya muda mrefu ya taifa kama vile Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga jamii yenye usawa, fursa sawa za kiuchumi na maendeleo jumuishi kwa wananchi wote.

Kupitia programu kama Samia Ardhi Kliniki, serikali na wadau mbalimbali wanaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi sawa katika kumiliki rasilimali muhimu kama ardhi, jambo ambalo linachangia kukuza maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI