Na Matukio Daima Media Morogoro
JITIHADA za kuwaokoa mama lishe wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu zimeanza kuzaa matunda baada ya kampuni ya Vinywaji baridi ya Coca-Cola Kwanza kwa kushirikiana na Oryx Gas na Manispaa ya Morogoro kuzindua Soko la kisasa la Chakula katika Stendi ya Mabasi ya Msamvu lenye vibanda 50 vya kisasa na salama.
Soko hilo limeanzishwa chini ya Mradi wa Mwanamke Shujaa, unaolenga kuwawezesha wanawake zaidi ya 450 wa Mkoa wa Morogoro huku wanawake 150 wa Msamvu wakiwa sehemu ya wanufaika wa kwanza wakitokea eneo la Msamvu.
Mbali na vibanda, Oryx Gas imetoa mitungi 150 ya gesi yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 11 ili kuchochea matumizi ya nishati safi na kuondoa utegemezi wa kuni na mkaa sambamba na mabenchi ya kisasa na viti vyake yaliyotengenezwa Kwa plastiki iliyochakatwa badala ya mbao au miti.
Mkurugenzi wa Mahusiano ya Jamii kutoka kampuni ya Coca-Cola Kwanza, Salum Nasoro, alisema mradi huo umejikita katika kutoa mafunzo ya ujasiriamali, afya ya jamii, usimamizi wa fedha na maendeleo binafsi ili kuhakikisha wanawake wanaendesha biashara zao kwa tija na usalama.
Balozi wa nishati safi, Jenepha Mosha, alisema gesi Imekuwa inapunguza maradhi yanayotokana na moshi wa kuni na mkaa, inalinda mazingira na kupunguza gharama kwa muda mrefu.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Khaled MATENGO alisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni kipaumbele cha kitaifa na akawataka wanawake kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 kuimarisha mitaji yao.
Aidha akawaasa wanaume kuendelea kuwaunga mkono wanawake kufikia mafanikio yao na kukua kiuchumi.
Baadhi ya Wanawake walionufaika akiwemo Sarah Nyamiti na Aisha Abdalah wametoa shukrani kubwa Kwa wadau hao wakisema sasa wanafanya kazi katika mazingira salama, yenye hadhi na yenye kuongeza kipato.



















0 Comments