Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same wamesisitizwa kuongeza uwajibikaji, kuimarisha usimamizi wa mapato na miradi ya maendeleo, pamoja na kuhakikisha wanatatua kero na changamoto za wananchi kwa wakati. Vilevile, wamekumbushwa kuhakikisha wanalinda na kusimamia kikamilifu mapato ya Halmashauri ili kuendeleza kupata hati safi kutoka kwa Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).
Maelekezo hayo yametolewa hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa Baraza la Kwanza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Ponciano Kirumbi alisema kuwa madiwani wanapaswa kuwajibika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi huku wakizingatia maadili ya utumishi wa umma.
Katika baraza hilo pia ulifanyika uchaguzi wa viongozi, ambapo Bw. Yusto Mapande alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri na Bw. Rashid Jasper kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, aliwahimiza madiwani kubuni vyanzo vipya vya mapato, kusimamia kikamilifu fedha za Halmashauri na miradi ya maendeleo, pamoja na kuwa mabalozi wa amani katika kata zao.
Akifunga baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri, Bw. Yusto Mapande, aliwashukuru madiwani wote waliompa kura na kuahidi kuwa baraza hilo litatoa ushirikiano kwa kila mmoja katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kikamilifu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Same Bw. Abdallah Mnyambo aliwataka viongozi wa serikali na wananchi kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha vurugu, likiwemo suala la maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 mwezi huu, na badala yake kuendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano ndani ya Wilaya ya Same.
Hatua hii inalenga kuimarisha misingi ya uongozi bora na kuleta maendeleo endelevu katika Wilaya ya Same.









0 Comments