Arusha,
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Novemba 27, 2025 alitembelea Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha kujifunza na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara.
Akiwa katika ziara hiyo, alisema kuwa “Uhifadhi ni msingi wa uhai, uchumi, utalii na ni fahari ya Taifa letu.” Amesisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika kulinda rasilimali za Taifa kwa kuwa wao ndiyo walinzi wa awali wa rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Waziri Kijaji alihimiza dhamira ya Tanzania kuwa namba moja katika utalii Afrika na duniani, akibainisha kuwa nchi ina misingi yote ya kufanikisha lengo hilo.
Ameielekeza Menejimenti ya TANAPA kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza ubora wa huduma na ulinzi wa rasilimali.
Amesema Serikali inalenga kufikia watalii milioni 8 ifikapo 2030, hivyo taasisi za wizara, ikiwemo TANAPA, zina wajibu wa kuhakikisha lengo hilo linatimia kupitia uimarishaji wa askari, vituo, vifaa, matumizi ya teknolojia na ubunifu wa vivutio vipya.
Aidha, ameagiza kuimarishwa kwa juhudi za kutangaza vivutio vya Kanda za Magharibi, Kusini na Mashariki. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande (Mb), amesema uhifadhi ni heshima ya nchi na jukumu hilo limekabidhiwa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu, hivyo maafisa wanapaswa kulinda hifadhi saa 24 kwa weledi na uzalendo.
Pia amesisitiza maboresho ya miundombinu ili kuwa rafiki kwa watalii. Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Nassoro Kuji, amesema ujio wa Waziri umeongeza chachu ya kuimarisha uhifadhi, akibainisha kuwa TANAPA itaendelea kulinda bioanuai, kuboresha mifumo ya ulinzi na kusimamia rasilimali kwa teknolojia za kisasa.
Katika ziara hiyo Waziri Kijaji aliambatana na Naibu Waziri Hamad Chande, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas na Wakurugenzi wa Wizara, ambapo walitembelea Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara kujionea vivutio na shughuli za utalii.





.jpg)






0 Comments