Na Ashrack Miraji Matukio Daima
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa sahihi wanapokwenda kujisajili katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ili kuepusha usumbufu na changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye, wakati wa kufanya marekebisho ya taarifa zao.
Wito huo umetolewa leo Novemba 27,2025 jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA James Kaji wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kibali maalum kilichotolewa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia maombi ya mabadiliko ya taarifa.
Amesema huduma ya mabadiliko ya taarifa imekuwa ikitolewa kwa watu waliojiandikisha katika mfumo wa NIDA kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Amefafanua kuwa kwa kipindi kirefu, NIDA ilipokea maombi mengi ya mabadiliko ya taarifa ambayo hayakuweza kushughulikiwa kutokana na kutokidhi matakwa ya kisheria na taratibu zilizokuwapo ambapo baadhi ya maombi hayo yalitoka kwa watu waliotumia nyaraka za kughushi au kutoa taarifa za udanganyifu walipojisajili, jambo lililozuia mabadiliko yao kufanyika.
Amesema kutokana na changamoto hizo, Serikali imetoa kibali maalum cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba 2025, kwa ajili ya kushughulikia maombi yote ambayo awali hayakuweza kufanyiwa kazi ambapo kibali hicho kinahusu makundi maalum yenye changamoto za taarifa, likiwemo kundi la waliofukuzwa kazi kutokana na kutumia vyeti vya kughushi ambavyo pia walivitumia kujisajili NIDA.
Makundi mengine yaliyojumuishwa katika kibali hicho ni pamoja na watu waliotumia majina ya wengine kupata vyeti vya elimu, wale waliotoa taarifa za uongo katika usajili wa NIDA, pamoja na raia wa Tanzania ambao walijisajili kama wakimbizi Hivyo amewataka makundi hayo kufika katika ofisi za NIDA za wilaya ili kupata huduma.
Aidha Kaji amesisitiza kuwa waombaji wote wanapaswa kwenda na nyaraka muhimu kulingana na aina ya tatizo lao huku akitaja baadhi ya nyaraka hizo kuwa ni pamoja na vyeti halisi vya elimu, cheti cha kuzaliwa kilichohakikiwa na RITA, deed poll iliyosajiliwa na gazeti la Serikali, na nyaraka nyingine ambazo zinaweza kuhitajika ili kuthibitisha taarifa sahihi.
Aidha, amebainisha kuwa si kila ombi litafanyiwa kazi, bali ni yale tu yatakayokidhi vigezo vilivyowekwa baada ya kuwasilishwa kwa vielelezo vinavyothibitisha mabadiliko yanayohitajika. Amesema mchakato huo utazingatia makosa ya awali, lakini pia utazingatia umuhimu wa kuimarisha usahihi wa taarifa katika mfumo wa taifa wa utambulisho.
Amesema kuwa kibali hicho kimetolewa kwa muda maalum wa mwaka mmoja pekee, hivyo wananchi wenye changamoto wanapaswa kuharakisha kwenda katika ofisi za NIDA kabla muda huo haujaisha. Alisisitiza kuwa muda ukipita, maombi mapya yatashughulikiwa kwa mfumo wa kawaida ambao una masharti makali zaidi.
Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wote nchini kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi wakati wa kujisajili kwa mara ya kwanza katika mfumo wa NIDA.
“kutoa taarifa za uongo ni kosa kisheria chini ya Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu, na hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi ya mtu atakayebainika kufanya udanganyifu”,Amesema.
Ameongeza kuwa usahihi wa taarifa ni msingi muhimu wa mifumo ya kitaifa, ikiwemo huduma za kifedha, afya, elimu, usalama na upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwani taarifa zisizo sahihi huathiri si tu mhusika, bali pia mifumo ya nchi na uendeshaji wa takwimu za kitaifa.
Sambamba na hayo NIDA imeeleza matarajio yake kwamba wananchi watatumia ipasavyo fursa hiyo adhimu iliyotolewa na Serikali ili kurekebisha taarifa zao kwa mujibu wa utaratibu







0 Comments