Header Ads Widget

WANAWAKE DODOMA WAJIKITA KUJENGA UCHUMI KUPITIA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WANAWAKE wa Jiji la Dodoma wameendelea kuonyesha hamasa kubwa katika kukuza uchumi wao kupitia Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, hatua inayochochea maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.

 Hayo yamebainika katika mkutano maalum uliofanyika Novemba 28, 2026, na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Priscila Mahundi (MB).

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe. Mahundi aliwapongeza wanajukwaa kwa kujenga mifumo imara ya ushirikiano na maendeleo ya kiuchumi, akisema majukwaa hayo yamekuwa daraja muhimu la kuongeza ujuzi wa fedha, uongozi na ujasiriamali.

“Majukwaa haya yamewafanya wanawake kuwa na uelewa mkubwa wa masuala ya fedha na kuwapa nguvu ya kuanzisha miradi yenye tija huu ndio mwelekeo tunaoutaka katika kujenga uchumi jumuishi,” amesema.

Aidha, Naibu Waziri alihimiza ushirikiano kati ya majukwaa, sekta binafsi na taasisi za kifedha ili kuongeza upatikanaji wa elimu ya biashara, masoko, teknolojia na mitaji rafiki kwa wanawake.

 Amesisitiza pia umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kupata mikopo.

Wakati wa majadiliano, mjasiriamali Priscila Manyenda ameeleza kuwa baadhi ya benki zimekuwa zikiweka masharti magumu, kama kulipia gharama za mwanasheria au kuwasilisha vyeti vya ndoa, jambo ambalo linawaathiri zaidi wanawake ambao hawajaolewa.

Amewahimiza wanawake kuendelea kujikita kwenye shughuli za kiuchumi kwa ujasiri na ubunifu.

“Jitihada hizi haziwanufaishi wanawake pekee, bali zinaimarisha familia, jamii na uchumi wa taifa wanawake wakiwezeshwa, taifa linaimarika,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. John Jingu, aliishukuru TAMISEMI na viongozi wa mkoa kwa kuratibu mkutano huo, akibainisha kuwa majukwaa hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwawezesha wanawake.

Mkutano huo umeonyesha kuwa uwezeshaji wa wanawake katika ngazi ya jamii unaendelea kukua kwa kasi, huku Dodoma ikionekana kuwa mfano wa mafanikio ya juhudi za wanawake kujitegemea kiuchumi.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI