Na Matukio Daima Media
SERIKALI ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu azimio lililopitishwa na Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) Novemba 26, 2025, ambalo lilizungumzia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini na kusababisha Kamisheni ya EU kusubirisha kwa muda utiaji saini wa Programu ya Ushirikiano ya Mwaka 2025 (AAP 2025) yenye thamani ya Euro milioni 156.
Serikali imesisitiza kuwa madai hayo hayana uthibitisho wa kuaminika na yametokana na taarifa za upande mmoja ambazo hazikupata fursa ya kupingwa au kupewa ufafanuzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Novemba 28, 2025, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaheshimu uhusiano baina yake na EU, ambao ni wa kihistoria, wenye zaidi ya nusu karne, na umejengwa juu ya misingi ya mazungumzo, kuheshimiana na kutokuingiliana katika masuala ya ndani ya kila upande.
Imeendelea kueleza kuwa imesikitishwa na hatua ya Bunge la EU kujadili na kupitisha azimio dhidi ya Tanzania bila kuipa Serikali fursa ya kusikilizwa, jambo ambalo linakwenda kinyume na kanuni ya haki ya kusikilizwa (Principal of Natural Justice) inayotambuliwa katika mifumo yote ya utawala bora duniani.
Aidha, Serikali imefafanua kuwa Tanzania ni Taifa huru linaloongozwa kwa misingi ya mamlaka kamili ya kitaifa, hivyo halifungwi na maamuzi ya Bunge la EU na kwamba kwa mujibu wa taratibu za kidiplomasia, uhusiano rasmi kati ya Tanzania na EU unasimamiwa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya na si Bunge lake, hivyo maazimio ya chombo hicho hayawi maagizo ya moja kwa moja kwa Serikali.
Kuhusiana na mijadala iliyoibuka kuhusu hatima ya misaada ya EU kwa Tanzania, Serikali imeweka wazi kuwa hakuna misaada iliyositishwa; badala yake, Kamisheni ya EU imesubirisha kwa muda utiaji saini wa Programu ya AAP 2025 ili kutoa nafasi ya mashauriano ya ziada.
Serikali imebainisha kuwa programu nyingine zote zilizokwishaidhinishwa na zinazoendelea kutekelezwa hazijaathiriwa na uamuzi huu; hivyo, taarifa zinazoenezwa kuhusu kusitishwa kwa misaada kwa ujumla wake hazina ukweli wowote.
Aidha, Serikali imetoa wito kwa Watanzania kupuuza taarifa potofu zinazoenezwa mitandaoni kuhusu suala hilo.






0 Comments