MBUNGE wa Jimbo la Tunduru kaskazini na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo Mhe. Ado Shaibu Ado amesema kutokana na uchapakazi wa Waziri Mkuu mteule wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ni matumaini yake kuwa atasaidia katika usimamizi wa rasilimali za Taifa ili ziweze kuwa na mchango katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Shaibu ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 13, 2025 bungeni Mjini Dodoma akiunga Mkono pendekezo la Rais Samia Suluhu Hassan, kwa niaba ya wabunge wa Vyama pinzani Bungeni la kumteua Dkt. Mwigulu kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mhe. Shaibu amemuomba Mhe. Mwigulu pia kusimamia maboresho ya demokrasia nchini na kuipatia Tanzania Katiba mpya kwakuwa Tasnia ya siasa na vyama vya siasa vipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka leo Alhamisi mchana, Dkt. Samia Suluhu Hassan atamuapisha Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho Ijumaa Novemba 14, 2025 Ikulu Chamwino Mjini Dodoma majira ya saa nne kamili za asubuhi.








0 Comments