Header Ads Widget

WAHAMIAJI HARAMU 40 WANASWA SONGWE, WAMO WAPAKISTAN 7 WALIOKIUKA MASHARTI YA VIZA.



 Na Moses Ng’wat, Songwe.


Idara ya Uhamiaji mkoani Songwe imewakamata jumla ya watu 40, wakiwamo raia saba wa Pakistan waliobainika kukiuka masharti ya viza, kufuatia operesheni maalumu iliyofanyika kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 21, 2025 katika maeneo ya mpaka wa Tunduma Mkoani Songwe.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 22, 2025 na Kaimu Afisa Uhamiaji wa mkoa huo, Mrakibu wa Uhamiaji Rose Mulaga Magesa, imeeleza kuwa kati ya wahamiaji hao waliokamatwa 31 ni raia wa Ethiopia waliokutwa bila hati halali za kusafiria na kwamba tayari wamefikishwa mahakamani na kuhukumiwa.


Aidha, Magesa ameeleza kuwa wengine waliokamatwa ni raia tisa wa Pakistan, ambapo saba walinaswa kwa tuhuma za kuvunja masharti ya viza walizopewa wakati wa kuingia nchini.


"Hawa raia saba kati ya tisa wa Pakistan tuliwakamata kwa makosa ya kukiuka masharti ya viza kwani licha ya Viza kuelekeza kwenda Dar es Salaam, maeneo ya Mbweni kwa ajili ya matembezi, wao walikiuka masharti na kusafiri hadi mkoani Songwe kwa shughuli nyingine... ndiyo maana tukawakamata,” alifafanua Magesa.





Mrakibu wa Uhamiaji Magesa aliwataja raia hao na namba zao za pasipoti kwenye mabano kuwa ni, Khizar Hayat (JJ6171151), Muhammad Rehman Rasheed (GU9842383), Muhammad Raza (YB9899821), Araiz Chand (YB9899821), Ahmed Ali (TF1832401), Aqib Javed (GH8676622) na Mubashar Ali (YF796162).


Magesa alisema watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 18, 2025 katika nyumba ya wageni ya Elishadai Lodge, iliyopo mji mdogo wa Tunduma, wilayani Momba.


Idara ya Uhamiaji imeeleza kuwa watuhumiwa wote wapo salama na wanatarajiwa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya hatua zaidi za uchunguzi mara baada ya mahojiano ya awali kukamilika.


Idara hiyo pia imeonya wageni wanaoingia nchini kuzingatia kikamilifu masharti ya viza na vibali vya ukaaji ili kuepusha kuvunja sheria za nchi, huku ikiwasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa wanapobaini wageni wasioeleweka katika maeneo yao.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI