NA JOSEA SINKALA, MATUKIO DAIMA MBEYA.
Mheshimiwa diwani wa kata ya Nsalaga jimbo la Uyole mkoani Mbeya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UVCCM) wilaya ya Mbeya mjini Clemence Mwandemba amechukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi ya mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mbeya.
Clemence James Mwandemba mgombea nafasi ya Meya wa jiji hilo la kibiashara na kilimo angali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kubwa ya kuongoza Baraza la waheshimiwa madiwani wa Halmashauri amesema ametimiza haki yake ya kikatiba kugombea umeya wa jiji la Mbeya akiamini kwamba ana uwezo wa kuwatumikia wananchi wa jiji la Mbeya.
Kwa sasa mwanachama huyo wa CCM anasubiri mchakato wa ndani ya Chama chake ikiwa ataaminiwa na CCM na kisha kuchaguliwa na madiwani kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya jiji la Mbeya kuwa mstahiki Meya.
Kiongozi atakayechaguliwa kwenye nafasi ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya jiji la Mbeya anakabiliwa na kibarua cha kushirikiana na viongozi (madiwani), Chama (CCM na vyama vingine) na wananchi kwa ujumla kuhakikisha Halmashauri ya jiji inapiga hatua kimaendeleo ikiwemo kubuni vyanzo vipya vya mapato na bila kuwaumiza wananchi, kusimamia vema fedha za Umma, kuweka mazingira bora ya usafi wa jiji, kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi na kutibu suala sugu la upangaji bora wa mipango mji ya jiji hilo na uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika baadaye Novemba 30 mwaka huu 2025.








0 Comments