Header Ads Widget

WADAU WA KILIMO SONGWE WATETA MWELEKEO MPYA WA UZALISHAJI, VIJANA WATAJWA KULETA MAGEUZI.

 

Na Moses Ng’wat, Songwe.

WADAU wa kilimo mkoani Songwe wamekutana kujadili mwenendo wa sekta ya kilimo, kufanya tathmini ya uzalishaji wa 2025 pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya msimu wa kilimo wa 2026, huku msisitizo ukiwa ni namna ya kuwahusisha vijana katika shughuli za kilimo ili kuchochea mageuzi ya sekta hiyo.


Akifungua kikao hicho cha jukwaa la kilimo lililoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, leo Novemba 20, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wakazi wa mkoa huo wanategemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato na ustawi wa maisha.


Alisema pamoja na umuhimu huo, Songwe pia ni miongoni mwa mikoa inayotegemewa nchini katika kuongeza usalama wa chakula na kuchangia juhudi za Tanzania katika azma ya kulisha Bara la Afrika.


"Sekta ya kilimo ndiyo muhimili wa maendeleo ya mkoa wetu... Halmashauri zetu zinategemea kilimo kwenye makusanyo yake ya ndani, wananchi wetu wanategemea kilimo kupambana na umasikini, kupata kipato na kuimarisha usalama wa chakula, hivyo hatuwezi kuzungumzia maendeleo bila kujadili kilimo,” amesema Makame.



Katika kikao hicho, wadau wanajadili pia njia za kuongeza thamani ya mazao, upatikanaji wa masoko, mitaji, pamoja na kuimarisha kilimo hifadhi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, akitoa tathmini ya msimu wa kilimo uliopita, Makame amesema mkoa huo uliweza kufikia wa asilimia 74 pekee ya malengo ya uzalishaji kwa mwaka 2025, hali iliyotajwa kuhitaji mikakati mipya na ufuatiliaji wa pamoja kati ya wadau wote.



Alisisitiza umuhimu wa kuwahusisha vijana katika kilimo, akibainisha kuwa ndiyo kundi kubwa zaidi kwenye mkoa, lakini ushiriki wao umekuwa mdogo katika shughuli hizo za kilimo.

"Tunapaswa kujiuliza, tunafanya nini kwenye Halmashauri zetu ili kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia vijana kuingia kwenye kilimo, kwani  shughuli za kilimo zimeachwa kwenye kundi dogo hivyo  vijana wakishiriki kikamilifu, tutaona mageuzi ya kweli,” amesema Makame.

Wadau wameahidi kuendelea kushirikiana katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kuinua kilimo mkoani Songwe kwa kuangazia uzalishaji, teknolojia, masoko na ubunifu katika shughuli za kilimo.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI