Header Ads Widget

MAMIA WAJITOKEZA BONANZA LA IRINGA MOTOR SHOW ,DC SITTA APONGEZA


NA MATUKIO DAIMA MEDIA , IRINGA

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amepongeza hatua kubwa iliyochukuliwa na waandaaji wa Iringa Motor Show, akisema kuwa bonanza hilo limeanza kuwa kichocheo muhimu cha kukuza utalii ndani ya Wilaya ya Iringa na Mkoa wa Iringa kwa ujumla. 


Akizungumza leo katika viwanja vya Kihesa Kilolo wakati wa tamasha hilo la michezo, DC Sitta alisema kuwa uamuzi wa vijana na wadau kuandaa bonanza hilo umefungua ukurasa mpya katika jitihada za kutangaza vivutio vya utalii kupitia michezo ya mbio za magari.

Akitoa pongezi zake mbele ya mamia ya wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo, DC Sitta alisema bonanza hilo limeifanya Iringa kuwa kitovu cha kukusanya wapenda michezo ya magari kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.


 Alisema kuwa kuwaleta pamoja wadau wa michezo hayo si tu kunachochea burudani, bali pia kunatoa fursa kwa wageni na wenyeji kuona maeneo mbalimbali ya vivutio ndani ya wilaya.



Kwa mujibu wa Sitta, michezo ya mbio za magari ni sehemu ya vivutio vinavyoweza kuongeza idadi ya watalii ikiwa itaendelezwa kikamilifu. 


“Waandaaji wa Iringa Motor Show mmefanya jambo kubwa sana. Mnawavuta watu wengi, mnaibua vipaji, lakini muhimu zaidi, mnachochea utalii,” alisema DC Sitta.


 Aliongeza kuwa Serikali inaona umuhimu wa mabonanza kama hayo na itaendelea kuyapa kipaumbele kwa kuwa yanachangia uchumi wa eneo husika na taifa kwa ujumla.


Akitaja hatua zinazochukuliwa na serikali, DC Sitta alisema kuwa eneo la Kihesa Kilolo tayari limeshatengwa kirasmi kuwa sehemu ya shughuli za kitalii kupitia mradi wa kuendeleza utalii kusini .



Alisema eneo hilo litaendelea kuboreshwa ili liwe na mvuto wa kudumu na kuwa kivutio kikubwa kwa wageni na wawekezaji katika sekta ya utalii na michezo.


“Tutaendelea kuhakikisha eneo hili linaboreshwa, linapimwa, na linakidhi vigezo vya kuwa moja ya maeneo ya kimkakati kwa ajili ya shughuli za burudani na utalii. Hii ni fursa kwa vijana na wote wanaojikita katika sekta ya utalii kuungana nasi kubadilisha sura ya Iringa,” alisema.


Aidha, DC Sitta aliwataka wadau wa utalii, wafanyabiashara, na makampuni binafsi kuendelea kujitokeza kudhamini mabonanza kama haya ili yawe na kasi na mvuto mkubwa zaidi. Alisema udhamini wa kutosha utawezesha matukio hayo kufanyika mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa zaidi, hali itakayoongeza mapato na ajira katika mji wa Iringa.



Katika hotuba yake, DC Sitta pia aliipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema imeweka misingi thabiti ya kuimarisha utalii nchini kupitia programu mbalimbali, ikiwemo kuzindua filamu na makala za kimataifa zinazotangaza Tanzania. Alisema mwelekeo huo umetia chachu katika maeneo yote ya nchi, na Iringa ni miongoni mwa wanufaika wakubwa kutokana na rasilimali na vivutio ilivyonavyo.


Kwa upande mwingine, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) na Mkuu wa Wilaya ya Iringa mstaafu, Richard Kasesela, hakuficha hisia zake kuhusu bonanza hilo. Kasesela alisema kuwa amevutiwa na ubunifu na juhudi zilizowekwa na waandaaji wa Iringa Motor Show. Aliwashauri vijana na wadau wasichoke bali waendelee kuandaa matukio hayo mara kwa mara, kwani yana mchango mkubwa sio tu katika kukuza utalii bali pia kuinua uchumi wa watu wa Iringa.


“Mimi ni mdau wa michezo, nimefurahi sana kuona vijana wa Iringa wanafanya jambo kubwa kama hili. Naahidi kushirikiana nanyi kadri ninavyoweza ili bonanza hili liwe kubwa zaidi ya hapa lilipoanza,” alisema Kasesela.



Akitoa taarifa za maandalizi na malengo ya bonanza hilo, Mratibu wa Iringa Motor Show, Amjad Khan, alisema kuwa hafla hiyo imebeba kaulimbiu “Iringa Yetu, Michezo Yetu.” 


Alisema kaulimbiu hiyo inabeba dhamira ya kuunganisha wakazi wa Iringa kupitia michezo, burudani, ubunifu na utalii. 

Alifafanua kuwa lengo la bonanza ni kuibua vipaji vipya, kuimarisha michezo ya mbio za magari na mingineyo, pamoja na kuongeza mwamko wa vijana kujikita katika shughuli zenye tija.



Amjad Khan alisema kuwa Iringa Motor Show haitakuwa tukio la mara moja, bali ni mpango endelevu utakaofanyika mara kwa mara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Alisema wanatarajia kuongeza idadi ya washiriki kutoka mikoa mingine na hata nchi jirani, ili kulifanya bonanza hilo kuwa la kitaifa na baadaye kimataifa.


Bonanza la mwaka huu lilikusanya washiriki kutoka Iringa na nje ya Mkoa wa Iringa  huku watu wengi wakifurika kushuhudia magari mbalimbali yaliyoshindanishwa katika mbio hizo. Tukio hilo lilipambwa na burudani za wasanii wa ndani, maonesho ya bidhaa, chakula, michezo ya watoto na fursa za kibiashara.


Kwa ujumla, tukio la Iringa Motor Show limeonesha kuwa Iringa ina nafasi kubwa katika kukuza utalii kupitia michezo, ubunifu na ushirikiano wa wadau. Matumaini yameongezeka kwamba mabonanza yajayo yatakuwa makubwa zaidi, yakichochea uchumi na kuongeza pato kwa wananchi wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI