Na. Philipo Hassan - Fort Ikoma - Serengeti.
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa majeshi (Mstaafu) Jenerali George Waitara leo Novemba 20, 2025 imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa uwanja wa Gofu “Serengeti National Park Golf Course” uliopo eneo la “Fort Ikoma” nje kidogo ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, mradi utakaoleta mapinduzi katika sekta ya utalii wa michezo nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Jenarali Waitara alisema “ Tumeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huu kwani hadi sasa ujenzi wa mashimo yote 18 umekamilika kwa asilimia 92, huku kazi ya kuotesha nyasi aina ya “Bermuda grasses” kwenye maeneo ya fairway ikiendelea ambapo mfumo wa umeme na umwagiliaji umeshakamilika.”
“Ukamilikaji wa mradi huu muhimu kwa Taifa utachochea ukuaji wa sekta ya utalii wa michezo nchini ambapo maelfu ya watalii watatembelea nchi yetu kwa ajili ya kushiriki utalii wa michezo Serengeti na kupelekea Serikali kukuza pato la Taifa, kuongeza idadi ya watalii, kuongeza ajira (Tourism Multiplier Effects) pamoja na ushiriki wa jamii katika michezo,” aliongeza Jenerali Waitara.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mhandisi Mshauri, Dkt. Richard Matolo alieleza kuwa uwanja huo una jumla ya mashimo 18 ambayo ni sehemu ya mradi mkubwa unaojumuisha uwanja wa ndege wa Fort Ikoma, ujenzi wa “waiting lounge,” nyumba za kulala wageni, “Clubhouse” kubwa na michezo mingine ya burudani kama tenesi.
“Kazi nyingine zilizofanyika ni ujenzi wa barabara ya kilomita 5.2, mabwawa manne makubwa ya kuhifadhi maji, uvutaji wa umeme wa TANESCO kutokea Wilayani Mugumu, uchimbaji wa visima virefu viwili, ujenzi wa “Power House” , mfumo mkubwa wa umwagiliaji pamoja na maeneo ya maegesho ya magari kati ya 100 na 150”, alieleza Dkt. Matolo
Naye, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti alisema kuwa mradi huo ni wa kipekee duniani kutokana na mazingira yake ya asili ambapo wachezaji wa gofu watakuwa na uwezo wa kuona wanyamapori kwa mbali wakati wakicheza. Pia uwanja huo utakuwa miongoni mwa viwanja virefu zaidi duniani, ukiwa na urefu wa takribani kilomita 7.065 na “Pars” 72 zilizogawanywa katika mashimo 18.
“Mradi huu unatarajiwa kuleta manufaa makubwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na hifadhi jirani kama vile Hifadhi za Taifa Kisiwa cha Saanane, Rubondo na Burigi–Chato, kutokana na mipango ya kuziunganisha kupitia usafiri wa maji kwenye Ziwa Victoria hasa Ghuba ya Speke iliyopo eneo la Nyatwali. Jitihada hizi zitaimarisha utalii wa majini na kuongeza siku za wageni kukaa hifadhini, hivyo kuongeza pato la Taifa”, aliongeza Kamishna Msumi.
Bodi ya Wadhamini TANAPA imeipongeza Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) inayoongozwa na Kamishna wa Uhifadhi, CPA Musa Nassoro Kuji pamoja na Menejimenti ya Kanda ya Magharibi na Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kusimamia mradi huo wenye manufaa mapana kwa Taifa.















0 Comments