![]() |
| Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Dk. Mboni Rezegea(katikati) na Mwenyekiti wa PATA (kushoto) Hermes Damian na Katibu Abdullah Saiwaad wakizungumza na waandishi wa habari |
Na Hellen Stanslaus
JAMII imeaswa kujikita katika usomaji wa vitabu ili kujiongezea maarifa zaidi.
Rai hiyo imetolewa Novemba 19 Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji wa Vitabu(PATA) Hermes Damian alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho ya vitabu yatakayofanyika kuanzia Novemba 21 hadi 26.
“Jamii ijikite katika usoamaji wa vitabu ili kujiongezea maarifa zaidi, kwa wiki soma kurasa tano za kitabu utakuwa mwingine kabisa
“Tuwe wajenzi wa taifa tunalotaka kwa kufanya jitihada za kuhakikisha tunakuwa na morari ya kuwajenga pia watoto na vijana wetu katika usomaji,” amesema Hermes.
Ameeleza kuwa kitabu ni suluhu ya mambo mengi na kwamba maonyesho hayo ya 32 ya Kimataifa ya vitabu ni fursa ya kuiambia dunia kuwa Tanzania ina maarifa lukuki.
![]() |
| Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishashaji wa Vitabu Hermes Damian akizungumza na waandishi wa habari |
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Nchini(TLSB) Dk. Mboni Ruzegea amesema lengo la maonyesho hayo ya vitabu ni kunadi historia ya lugha na tunu ya taifa kupitia kazi za waandishi nchini, kuonyesha umma utajiri wa maandishi, utamaduni, Sanaa na historia kama taifa, kuhamasisha jamii kuhusu usomaji wa vitabu ili kupanua maarifa na fikra.
“Tunazo taarifa kwamba kuna machapisho mengi yapo lakini hayajulini hivyo maonyesho haya yatatumika kama jukwaa la kuwezesha haya na mengine,” amesema Dk. Ruzegea.
Ameweka wazi kwamba hivi sasa usomaji wa vitabu duniani uko mbele kwani mambo mengi yanafanyika Kidijitali hivyo kama nchi tusipokuwa makini tutaachwa nyuma.
Ameiasa jamii ihakikishe inatumia maonyesho hayo kwa manufaa yao na taifa. Kauli mbiu ya maonyesho hayo yatakayowashirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi ni maktaba ya kesho leo.







0 Comments