Header Ads Widget

SIRRO ATANGAZA KIAMA KWA MAJAMBAZI ZIWA TANGANYIKA

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro amesema kuwa serikali ya mkoa itachukua hatua madhubuti kudhibiti ujambazi katika ziwa Tanganyika ambapo kuanzia sasa jeshi la ulinzi wa wananchi Tanzania (JWTZ) litaongezwa katika kufanya doria ziwa Tanganyika.

Balozi Sirro alisemaa hayo akizungumza na wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi katika Mwalo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa changamoto ya ujambazi katika ziwa Tanganyika sasa imefika mwisho na kwamba watafanya doria kuhakikisha wanasafisha majambazi wote ili wavuvi na watu wenngine waweze kufanya shughuli zao kwa hali ya usalama na amani.

Katika mkutano huo Balozi Sirro ametangaza kutoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa za watu wanaoajihusisha na masuala ya ujambazi wanaoteka boti na vifaa vya wavuvi na kwamba taarifa hiyo itachukuliwa kuwa siri na atakayetoa taarifa hiyo atalindwa.


Awali akitoa kero zinazowakabili wavuvi katika Mwambao wa ziwa Tanganyika Mwenyekiti wa Wavuvi mkoa Kigoma, Francis John alisema kuwa jumla ya mashine 52 za boti za uvuvi zimeibwa kutoka kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa tuhuma kubwa za wizi huo zinafanywa na watu kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wakishirikiana na baadhi ya watanzania ambapo maeneo ya Lubengera na Nanga wilaya ya Uvinza yakielezwa kuwa vinara wa kutumika kwa wizi huo.


Kwa upande wake mmoja wa wavuvi anayefanya shughuli zake kwenye mwalo huo wa Katonga Manispaa ya Kigoma Ujiji, Fortunatus Mtuli alisema kuwa wizi huo kwa kiasi kikubwa unachangiwa na polisi kushindwa kufanya doria kulinda wavuvi na mali zao lakini wamekuwa hodari katika kukamata vitenge na vipodozi vinavyoingizwa kwa njia ya magendo kutoka DRC na Burundi kwa njia ya boti.


 

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI