Na Moses Ng’wat, Mbozi.
Mfanyabiashara, Rister Wiliam Mwasile, mkazi wa Kijiji cha Lumbila, Kata ya Luanda wilayani Mbozi, amekamatwa akidaiwa kuuza mbolea ruzuku aina ya DAP kwa bei ya juu kinyume na mwongozo wa serikali, huku mume wake,Hemed Gira, akitoroka kimafia katika harakati za kumkamata.
Wenza hao wanaomiliki duka la pembejeo la Gira Agrovet katika kijiji hicho, wamebainika kununua namba za wakulima na kuzitumia kuingiza taarifa kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea na kujipatia mbolea ambayo huwauzia wakulima kwa bei ya juu.
Katika operesheni iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Omari Makame, Novemba 24,2025, watuhumiwa hao walikutwa na mifuko 88 ya mbolea, kati ya hiyo 65 ni DAP, ambayo waliiuzia wakulima kati ya Sh. 90,000 hadi Sh. 95,000, huku bei elekezi ya serikali ikiwa Sh. 76,000.
Rc Makame ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, alibainisha kuwa watuhumiwa hao na baadhi ya wafanyabiashara wasio waadilifu wamekuwa wakitumia udanganyifu kupata mbolea ya ruzuku na kwenda kuilangua kwa wakulima kinyume cha sheria.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni wizi dhidi ya serikali na wakulima, na aliagiza vyombo vya usalama kumsaka mume wa mfanyabiashara huyo na kuanzisha operesheni endelevu za kudhibiti ulanguzi wa pembejeo mkoani.
Makame alitumia fursa hiyo kuwataka wakulima kuacha kuuza namba zao kwa walanguzi kwani kufanya hivyo ni kosa, huku akisisitiza kuwa mfuko wa mnolea aina ya DAP haupaswi kuuzwa kwa zaidi ya Sh. 76,000.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, alisema mkoa wa Songwe umepokea tani 9,800 za mbolea za aina mbalimbali na kwamba licha ya kuwepo changamoto ya upatikanaji wa mbolea ya DAP, tayari tani 22,000 za zimeingizwa nchini na zinaendelea kusambazwa.
Mwisho.








0 Comments