Header Ads Widget

SIRRO AFUNGUKA WAVUVI KUPORWA ZIWA TANGANYIKA

 

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MKUU wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewaonya watu wote wanaoijishughulisha na matukio ya ujambazi kwa kupora zana za wavuvi katika mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ambapo ametangaza kuwa serikali imeanza kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo.

Mkuu wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro (mwenye kofia kushoto) akitembelea na kukagua shughuli za uvuvi katika Mwalo wa Lubengera kijiji cha Msiezi wilaya ya Uvnza mkoani Kigoma ambapo pia alifanya mkutano wa hadhara na wananchi kufuatia matukio ya uporaji wa zana za uvuvi unaofanywa ziwa Tanganyika na kijiji kikiwa ni moja ya maeneo yanayokabiliwa na uporaji mkubwa wa zana hizo za uvuvi.

Balozi Sirro alisema hayo akizungumza na wananchi na wavuvi wa Mwalo wa Lubengera kijiji cha Msiezi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma alipotembea mwalo huo kukagua na kuzungumza na wananchi wa vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika akieleza hatua ambazo serikali imeanza kuchukua kukabiliana na hali hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa katika hatua za awali vikosi vya ulinzi na usalama ikiwemo polisi kikosi cha wana maji na jeshi la wananchi kikosi cha wana maji (Navy) watafanya doria ya pamoja katika mwambao wote wa ziwa Tanganyika kuhakikisha matukio ya uporaji wa zana za uvuvi mkoani humo hayatokei tena,

Mkuu wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msiezi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma akizungumzia masuala ya ulinzi na usalama wa ziwa Tanganyika kufuatia wimbi la uporaji wa zana za uvuvi katika mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ambapo kijiji hicho kimeathirika kwa kiasi kikubwa na matukio hayo.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa halmasgauri ya wilaya ya Uvinza na Halmashauri ya wilaya ya Kigoma zitashiriki katika mpango huo ambapo boti za polisi, jeshi na halmashauri hizo mbili zitahusika kusambazwa maeneo mbalimbali ya mwalo wa ziwa Tanganyika kuimarisha uvuvi huku akiwaonya wazazi kuhakikisha kuwa wanakanya watoto wao kwani watuhumiwa watakaokamatwa watashughuliliwa kikamilifu.

Mwalo wa uvuvi wa Lubengera kijiji cha Msiezi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma

Awali Mkuu wa wilaya uvinza, Dinnah Mathamani alisema kuwa Mwalo wa Lubengera ni miongoni mwa maeneo ambayo yamewekwa kwenye eneo la hatari kutokana na matukio ya mara kwa mara ya uporaji wa zana za uvuvi lakini tayari wameshaweka mipango kuhakikisha hatua mbalimbali za kudhibiti hali ya usalama zinachukuliwa ikiwemo kufanya doria.


Mkuu wa wilaya Uvinza Dinnah Mathamani akizungumza katika mkutano wa Mkuu wa mkoa na wananchi wa kijiji cha Msiezi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma

Mmoja wa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika mwalo huo, Yahaya Selemani alimweleza  Mkuu wa mkoa Kigoma kwamba uporaji zana za uvuvi unaofanywa na watu wanaotuhumiwa kutoka nchi ya jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakishirikiana na Watanzania kumewaathiri kiuchumi kwani wamekuwa waoga kuimarisha shughuli zao kutokana na mikopo ya benki wanayochukua.


Yahaya Selemani Mvuvi wa kijiji cha Msiezi Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma akieleza kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Simon Sirro (aliyekaa kulia) athari za uporwaji wa zana za uvuvi katika mwambao wa ziwa Tanganyika.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI