Header Ads Widget

SERIKALI YATOA ONYO KALI KWA VYOMBO VYA HABARI VYA NJE


Serikali imetoa onyo kali kwa baadhi ya vyombo vya habari vya nje vinavyochapisha taarifa kuhusu uchaguzi wa hivi karibuni bila kuzingatia misingi ya taaluma, usawa, haki na uwajibikaji. Imeeleza kuwa hatua hizo huenda zikaathiri amani na usalama wa taifa, hivyo ikavionya vyombo hivyo kuacha mara moja tabia hiyo.

Aidha, Serikali imewataka wananchi kuwa na subira wakisubiri ripoti ya tume maalum iliyoundwa kuchunguza chanzo cha maafa yaliyotokea wakati wa vurugu hizo. Imefafanua kuwa tume hiyo inapaswa kufanya kazi yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu yeyote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam, Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema vyombo vya habari vinapaswa kuihofia serikali ili kusikia upande wa pili wa taarifa kabla ya kuchapisha habari, badala ya kutoa taarifa za upande mmoja.


“Hata hivyo, katika kipindi hicho kulitokea vurugu zilizosababisha vifo vya raia na askari, pamoja na uharibifu wa mali za umma na binafsi. Natoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwaombea marehemu wapumzike mahali pema. Sasa suala hili tumeiachia tume ili ije na ripoti kamili kuhusu yaliyotokea,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa serikali inazitahadharisha taasisi za habari kutoka nje ya nchi kuepuka kuchapisha taarifa zisizo na uwiano, na badala yake zifuate maadili ya uandishi wa habari. Amesema serikali ipo tayari kutoa ushirikiano inapohitajika.

Pamoja na changamoto zilizopo, Msigwa amewapongeza waandishi wa habari wa ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya, akitaja uandishi wao kuwa wa kizalendo na wa uwajibikaji.


Ameitaka jamii kujiepusha na kusambaza habari za uchochezi ambazo zinaweza kuligawa taifa. Amesisitiza kuwa kwa sasa vita kubwa ni vita ya taarifa, inayolenga kuibua taharuki na kuathiri uchumi wa nchi.

Msigwa amesema Watanzania wanataka amani, lakini kuna baadhi ya watu wanaotumia taarifa potofu kutaka kuvuruga utulivu wa nchi ili kunufaika kisiasa na kiuchumi endapo hali itadhoofika.

Serikali imeeleza kuwa hadi sasa hali ni shwari, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kulinda watu na mali zao. Hivyo, Watanzania wametakiwa kuendelea kuwa watulivu, kwani Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazotarajiwa kukua zaidi kiuchumi barani Afrika.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI