Msanii wa rap Nicki Minaj, anayeishi Marekani na ambaye ameuza mamilioni ya rekodi, amemuunga mkono hadharani Rais Donald Trump katika madai yake kwamba Wakristo wanakabiliwa na mateso nchini Nigeria.
“Nchini Nigeria, Wakristo wanalengwa,” Minaj alisema Jumanne katika hafla ya Umoja wa Mataifa iliyoandaliwa na Marekani, akiongeza kuwa: “Makanisa yamechomwa, familia zimeng’olewa mizizi… kwa sababu tu ya jinsi wanavyosali.”
Hii inafuatia vitisho vya hivi karibuni vya Trump vya kutaka kutuma wanajeshi kwenda Nigeria “wakiwa na bunduki tayari kufyatua risasi” iwapo serikali yake “itaendelea kuruhusu kuuawa kwa Wakristo”.
Lakini ikulu ya Nigeria inasema kwamba ukatili mpana ambao umekuwa ukiikumba nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa muda mrefu unawaathiri watu wote, bila kujali asili au imani yao.
Minaj, ambaye jina lake halisi ni Onika Tanya Maraj-Petty, alisema kwamba kutaka kulindwa kwa Wakristo nchini Nigeria “si suala la kuegemea upande mmoja au kuwagawa watu,” bali ni kuhusu “kuunganisha ubinadamu.”
“Hili linahusu kusimama dhidi ya ukosefu wa haki. Ni kuhusu kile ambacho nimekuwa nikikisimamia siku zote,” aliongeza akiwa pamoja na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz.
Msanii huyo wa rap mwenye umri wa miaka 42 alimshukuru Trump kwa “kulipa suala hili kipaumbele .”
Alielezea Nigeria kama “taifa zuri lenye mila za kina za imani” na hata akaonesha kuthamini mashabiki wake walioko nchini humo.
Waltz alimshukuru Minaj kwa “kutumia jukwaa lake kubwa kuangazia ukatili dhidi ya Wakristo nchini Nigeria.”
Kwa miezi kadhaa, wanaharakati wa mrengo wa kulia na wanasiasa mjini Washington wamekuwa wakidai kwamba wanamgambo wa kiislamu wamekuwa wakiwalenga Wakristo nchini Nigeria.
Wataalamu wanasema kwamba migogoro ya kusababisha vifo mara nyingi hutokana na rasilimali muhimu kama ardhi na maji, au huongozwa na mvutano wa kikabila, badala ya dini.






0 Comments